ASKOFU: RAIS MAGUFULI MAJIPU UNAYOYATUMBUA WEWE NI MAJIPU MADOGO MADOGO...
Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth
Magufuli jana Sikukuu ya Pasaka, waliungana na Waumini wa Kanisa la
Africa Inland – Tanzania Dayosisi ya Pwani Pastorate ya Magomeni kusali
Ibada ya Pasaka.
Katika Ibada hiyo Askofu wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Baba
Askofu Charles Salalah aliongoza maombi ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli
ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza nchi vizuri na
alimpongeza kwa kazi kubwa ya kurekebisha mambo yote yasiyofaa nchini
ikiwemo kuwaondoa viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya na kufuja mali
za umma.
“Mhe. Rais unafanya kazi kubwa ya kutumbua majipu, majipu unayoyatumbua
wewe ni majipu madogomadogo yaliyotokana na jipu kuu ambalo ni dhambi za
mwanadamu, na jipu hili lilitumbuliwa na Bwana Yesu, kwa hiyo sisi
Wakristo wenzako na waumini wengine tunakuombea sana na tunakuunga mkono
katika kazi hii nzito ya kutumbua majipu haya madogomadogo ya watumishi
hewa, mishahara hewa, mikopo hewa na mengine mengi” alisema Askofu
Charles Salalah.
Akizungumza katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli aliwashukuru Wakristo
wa Kanisa la Africa Inland na waumini wa madhehebu mengine ya dini kwa
kuendelea kumuombea na ameomba maombi hayo yaendelee, na pia waiombee
nchi iendelee kuwa na amani, umoja, mshikamano na watu wachapa kazi.