ASKOFU GWAJIMA AKARIBISHWA KUENDESHA HUDUMA YA USAFIRI WA TRENI TANZANIA

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekaribishwa kuwa anaweza kuendesha huduma ya usafiri wa treni na kutaka wadau wengine wenye nia kama hiyo wajitokeze.

Katika ibada iliyofanyika juzi, Askofu Gwajima aliwaambia waumini wake kuwa amedhamiria kununua treni ya umeme itakayogharimu Sh11 bilioni, baada ya Rais John Magufuli kuzindua mradi wa ujenzi wa reli pana (standard gauge) itakayokuwa na kasi zaidi ya treni ya sasa na uwezo wa kuchukua shehena kubwa.

Ujenzi wa reli uliozinduliwa na Rais Magufuli Aprili 12, utakamilika ndani ya miezi 30 na awamu ya kwanza itaanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, treni yake itakuwa na kasi ya kilomita 160 kwa saa, ikibeba mabehewa 100.

Msemaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Catherine  Moshi alisema kampuni hiyo  imebariki uamuzi huo wa kuwekeza katika usafiri wa reli, lakini askofu huyo anatakiwa kuomba kibali  Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

“Tunamkaribisha mchungaji, hii ni biashara kwetu na huyu ni mwekezaji tena wa ndani. Hatuwezi kumuangusha cha muhimu ni kufuata utaratibu tu,’’ alisema Catherine.
Powered by Blogger.