ZAIDI ya waumini wapya 500
wamemkubali Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wao kwa kuzamishwa ndani ya maji mengi
katika kanisa la Waadventista Wasabato katika Konferensi ya Mara.
Idadi hiyo imetolewa na Mwenyekiti
wa Konferensi ya Mara Mchungaji George Ojwang Ezekiel wilayani Tarime wakati
alipofanya mahojiano na mwandishi wa blog hii wakati akikagua Zahanati ya Tarime iliyoko
katika kanisa la Turwa mtaa wa Turwa Mjini Tarime.
Mchungaji Ojwang amesema kuwa idadi
hiyo imetokana na mahubiri ya Total Membership Involvement (TMI) yanayoendeshwa
kwenyen vituo 350 mkoa mzima wa Mara.
Amesema kuwa kupitia vituo hivyo
ambavyo vimeungamishwa na mahubiri ya Ushindi Hatimaye yanayorushwa Mubashara
kutoka kanisa la Mabatini Jijini Mwanza, waumini wapya zaidi ya 500 wamemkubali
Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa Maisha yao na kubatizwa.
"Tulitarajia kuwa na vituo 417
kama ilivyo idadi ya makanisa Mara Konferensi lakini kutokana na hali ya uchumi
baadhi ya makanisa yameshindwa kupata vifaa vya kuendeshea vituo vyao,"
amesema Mwenyekiti wa kanisa Mara Konferensi Mchungaji Ojwang.
Aidha katika hatua nyingine
mchungaji Ojwang akiambatana na katibu mkuu wa konferensi hiyo Mchungaji Enock
Sando, mkurugenzi wa Mawasiliano, mchungaji Joseph Matongo, mkurugenzi wa
Idara ya afya na mhazini wa jimbo hilo amefungua kituo cha afya Bukwe kilichoko
Wilayani Rorya baada ya kusimama kutoa Huduma kwa kipindi cha mwaka mmoja
huku akifanya ukaguzi katika zahanati ya Tarime iliyoko katika kanisa la Turwa
mjini Tarime.
"Kuanzia Leo kituo cha afya
Bukwe kimefunguliwa rasmi ili kianze kutoka Huduma kwa wagonjwa, nitumie fursa
hii kuwataarifa wananchi na wakazi wa Tarime na Rorya kwenda kupata Huduma ya
matibabu katika vituo vyetu vilivyo karibu nao maana siyo kuwa tunatoa Huduma
za kitabibu tu Bali waganga huomba kabla ya kutoa Huduma," alibainisha.
Kituo cha afya Bukwe kilifungwa
baada ya kuonekana kuwa na mapungufu kadha wa kadha na kuulazimu uongozi
kukifunga ili kukiweka katika mazingira mazuri ya utoaji Huduma kwa wagonjwa
jambo ambalo sasa limetekelezwa kwa kiwango kinachostahili.
Aidha amewataka wachungaji wa mitaa,
wazee wa makanisa na wakurugenzi makanisani kuhudhuria mkutano wa GAiN Mara
konferensi utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu katika kanisa la Tarime kati
Wilayani Tarime kwa muda wa siku tano.
"Viongozi hawa wakihudhuria
mkutano huu utawajengea uwezo wa kuenenda na wakati katika kutoa utume wetu
tulioitiwa, na wasipange kukosa mikutano hiyo," alisema Mchungaji Ojwang.
|