MKUU WA SHULE YA SEKONDARI AJINYONGA...CHANZO UPWEKE BAADA YA ULEVI
MKUU
wa Shule ya Sekondari Tumuli katika Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida,
Richard Makala (58) amejinyonga kwa kamba kutokana na kile
kinachodhaniwa kuelemewa na upweke.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba, amesema mjini Singida kuwa, Makala alijinyonga jana saa 1 asubuhi.
Ameeleza kuwa Makala alikutwa amejinyonga kwa kutumia kamba
iliyotengenezwa kwa vipande vya chandarua iliyofungwa juu ya mti umbali
wa mita 130 kutoka nyumbani kwake.
Amesema, chanzo cha tukio hilo hakijajulikana na kwamba hakuna mtu au
watu wanaoshikiliwa kutokana na tukio hilo na kuongeza kuwa polisi
inaendelea na upelelezi kubaini kilichomsibu mwalimu huyo.
Hata hivyo, Mjumbe wa Bodi ya shule hiyo, Mabruki Ng’ui amelisema
mwalimu huyo alikuwa anaishi peke yake kwa muda mrefu baada ya mkewe
ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Tanzania
(KKKT) Kitusha wilayani Iramba kuamua kutengana naye kutokana na
unywaji pombe.
"Huyu bwana amekuwa kwenye ndoa ya jina tu maana mke wake amekuwa
akiishi mbali naye kwa kipindi kirefu sana, amekuwa mpweke kwa muda
mrefu mno huenda hicho ndicho kilichosababisha ajitoe roho yake,"
amesema Mjumbe huyo wa Bodi.
Makala ni mzaliwa wa kijiji cha Ndago, wilayani Iramba na anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwake.
Ameacha mjane na watoto watano.
IMEANDIKWA NA ABBY NKUNGU-HABARILEO SINGIDA