HAKUTA KUJA KUTOKEA UPUNGUFU WA SUKARI NCHINI – WAZIRI MKUU
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema
kwamba Tanzania haitapata upungufu wa sukari kutokana na kuanza kwa
uzalishaji wa sukari kwa viwanda vya ndani.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali
la Mbunge Suleiman Ahmed Sadick alipotaka ufafanunuzi namna ambavyo
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga ikiwa tatizo la upungufu wa sukari
litajirudia tena.
“Tayari
Viwanda vya ndani vimeanza uzalishaji wa sukari ambapo kufikia mwisho
wa mwezi Machi mwaka huu ambao ndio mwisho wa msimu tutakuwa tumefikia
lengo la uzalishaji wa sukari kwa nchi nzima,” alifafanua Majaliwa.
Aidha,
Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara kutoweka vyakula ndani ili
kuviuza kwa bei ya juu baadae, badala yake amewataka kuuza vyakula hivyo
ili kuongeza upatikanaji wa chakula nchini, kwani uongezaji wa bei wa
vyakula unaumiza wananchi wa kipato cha chini na kati.
Katika
kukabiliana na tatizo la ukame kwa baadhi ya maeneo hapa nchini, Waziri
Mkuu amewataka wakulima kutumia kipindi hiki ambacho baadhi ya maeneo
yanapata mvua kwa kupanda mazao ya muda mfupi ambayo pia mazao hayo
yataweza kutumika kwa msimu ujayo.