WALIMU WATATU MBARONI KWA KUPOKEA MISHAHARA MIWILI
Walimu watatu mkoani Mwanza wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la
kukimbia vituo vyao vya kazi na kufanya kazi shule binafsi huku
wakiendelea kupokea mishahara ya serikali.
Taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa Mwanza imewataja walimu hao
waliokamatwa jana asubuhi katika mtaa wa Buhongwa wilaya ya Nyamagana
jijini Mwanza,kuwa ni pamoja na Richard Mgendi (30), Rwiza Ntare (27) na
Gilbert Makwaya (33).
Walimu hao kila mmoja ana story yake kama ifuatavyo:-
Mwalimu Richard Mgendi alikuwa akifundisha shule ya sekondari ya Misasi
wilayani Misungwi, mwaka 2012 alimuaga mkurugenzi wa wilaya hiyo kuwa
anakwenda kusoma Masters ya lugha (Linguistic) katika chuo kikuu cha
Mtakatifu Augustino, kwa kipindi chote hicho inadaiwa mwalimu huyo
alikwenda kusoma na alipomaliza hakurudi katika shule yake ya awali bali
alikuwa akifundisha shule binafsi ya sekondari iitwayo Musabe iliyopo
Buhongwa huku akiendelea kulipwa mshahara kutoka serikalini.
Mwalimu Rwiza Ntare alikuwa akifundisha shule ya sekondari iitwayo
Kigongo sekondari iliyopo wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo mwaka
2015, alimuaga mkurugenzi wake kuwa anakwenda hospitali ya rufaa ya
Bugando kupatiwa matibabu ya macho na vidonda vya tumbo lakini hakurudi
tena bali inadaiwa alikuwa akifundisha shule binafsi ya sekondari
iitwayo Musabe iliyopo mtaa wa Buhongwa huku akiendelea kulipwa mshahara
na serikali.
Mwalimu Gilbert Makwaya alikuwa akifundisha Runima sekondari iliyopo
maeneo ya Buhongwa na alimuaga mkurugenzi wa wilaya ya Nyamagana tarehe
27/09/2015 kuwa anakwenda kusoma Masters ya Hesabu katika chuo kikuu cha
Mwenge kilichpo mjini Moshi lakini hakwenda bali alikuwa akifundisha
shule binafsi ya Musabe iliyopo mtaa wa Buhongwa huku akiendelea kupokea
mshahara kutoka serikalini.
Walimu wote watatu wapo katika mahojiano na jeshi la polisi na pindi uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Jeshi la polisi linaendelea kuwatafuta baadhi ya walimu ambao wametoroka
lakini inadaiwa wapo katika shule hiyo binafsi ya Musabe huku
wakiendelea kulipwa mshahara na serikali pamoja na mkurugenzi wa shule
hiyo.