Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (katikati) pamoja na mshindi
wa medali ya dhahabu katika mbio za Standard Chartered Mumbai Marathon 2017 Bw.
Alphonce Felix Simbu wakiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) tuzo
aliyoipata Bw. Simbu katika mashindano ya Mumbai Marathon yaliyofanyika Januari
15 mwaka huu leo wakati wa hafla fupi ya kumpongeza jijini Dar es Salaam.
Picha/Habari na Genofeva Matemu
Wadau
mbalimbali wa sekta ya michezo nchini wametakiwa kujitokeza kudhamini michezo
nchini ili kuweza kurudisha utukufu wa mafanikio katika sekta ya michezo na
nchi kwa ujumla.
Rai
hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses
Nnauye wakati wa hafla fupi ya kumpokea na kumpongeza mshindi wa medali ya
dhahabu katika mbio za standard Chartered Mumbai Marathon 2017 leo Jijini Dar
es Salaam.
“Wadau
wa michezo jitokezeni tushirikiane kwa pamoja kuboresha michezo nchini na kurudisha
utukufu wa mafanikio katika sekta za michezo na nyingine ninazozisimamia kwani
ni sekta ambazo zina mvuto ndani ya jamii” amesema Mhe. Nnauye.
Aidha
Mhe. Nnauye ameipogeza kampuni ya Multi Choice kwa kujitolea na kuwa wazalendo
kuwekeza kwa mwanariadha Simbu ambaye amekua na mwanzo mzuri ambao utakua
chachu kwa vijana wengi nchini kuthamini na kujituma katika mashindano
mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa
upande wake mshindi wa medali ya dhahabu katika mbio za Standard Chartered
Mumbai Marathon 2017 Bw. Alphonce Felix Simbu amewataka wanariadha wenzake
nchini kufanya juhudi katika mazoezi ili kufikia mashindano ya dunia ya riadha
Tanzania itoe idadi kubwa ya washiriki katika mashindano hayo.
Naye
Katibu Mkuu Chama cha Riadha Tanzania Bw. Wilhelm Gidabuday amempongeza mshindi
wa medali ya dhahabu katika mbio za standard Chartered Mumbai Marathon 2017 Bw.
Simbu na kumtaka kuendelea kuwa kioo kwa wanariadha wenzake nchini.
|