WAANDISHI KUPIGWA KWENYE MSAFARA WA WAZIRI MKUU MSTAAFU, EDWARD LOWASSA MKOANI GEITA.



Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Edward Lowassa, jana akiwapungia mkono wananchi wa Geita akiashiria kuwasalimia wakati alipokuwa akipita kuelekea kata ya Nkome.
Msafara wa Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya chama cha demokrasia na Maendeleo chadema Edward Lowassa ukipita katika viunga vya mji wa Geita huku ukiwa umepokelewa na waendesha pikipiki maarufu kwa jina la boda boda.
Askali Polisi wakiwatawanya wananchi kwenye maeneo ya stendi  ya zamani Mjini Geita ambao walikusanyika kusalimiana na  Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya chama cha demokrasia na Maendeleo chadema Edward Lowasa.
Kamanda wa polisi wilaya ya Geita (OCD) Ally Kitumbo akiwatawanya wananchi ambao walikusanyika kwenye eneo la stendi ya zamani.
Msafara wa Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya chama cha demokrasia na Maendeleo (chadema) Edward Lowasa ukielekea kituo cha polisi.
Baadhi ya askali wakiwa katika majukumu yao ya kikazi.
Askari wakiwa wameweka ulinzi kwenye uzio wa Ngome ya makao makuu ya jeshi la polisi Mkoani Geita,ambapo kulikuwa kukifanyika maojiano ya Mhe,Lowasa na jeshi hilo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita, Mponjoli Mwabulambo akikanusha taarifa ya kukamatwa kwa ,Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya chama cha demokrasia na Maendeleo chadema Edward Lowasa.
Na Maduka Online
Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Edward Lowassa pamoja na  ujumbe aliokuwa amefatana nao jana walishikiliwa na jeshi la polisi mkoani Geita kwa mahojiano ambayo yalidumua kwa  zaidi ya masaa matatu, wakati akitokea mkoani Kagera.
Ni baada ya kufika stendi ya mabasi ya zamani Geita kwa lengo la kusalimiana na wananchi wakati akipita kuelekea kwenye kampeni za uchaguzi mdogo kata ya Nkome.
Tukio la kukamatwa kwa waziri mkuu huyo,lililoambatana na vipigo vikali kwa waandishi wa habari wawili,Valence Robert wa Chanel Ten na Joeli Maduka wa Storm Fm ambaye pia ni mmiriki wa mtandao wa madukaonline ya mjini Geiti lilitokea leo majira ya saa 9:30 jioni eneo la stendi ya zamani ya mabasi iliyopo katika kata ya kalangalala mjini Geita.
Lowassa ambaye alikuwa kwenye gari  yenye namba T 771 DEA aina ya V8 Land curuser na wenzake ambao ni Hamis Mgeja pamoja na Profesa Balegu walikuwa wakitokea mjini Bukoba kuelekea mjini Geita kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaofanyika katika kata ya nkome wilaya ya Geita Vijijini.
Kwa mjibu wa mwandishi Joel Maduka chanzo cha Lowassa kukamatwa kilitokana na na yeye kusimama kisha kuzungumza na wananchi waliokuwa wamekusanyika katika standi hiyo kumweleza changamoto zinazowakabili ikiwemo ugumu wa maisha na ukame kukithiri hali ambayo imesabauisha baadhi ya maeneo kukumbwa na njaa.
Hata hivyo saa chache kabla ya Lowassa kujibu kilio cha wananchi hao,kamanda wa polisi wilaya ya Geita(OCD)Ally Kitumbo alifika eneo hilo akiwa ameongozana na askari zaidi ya kumi waliokuwa na silaha za moto kisha kumwamuru Lowassa kwenda kituo cha polisi bila shuruti.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya wananchi waliamua kuandamana wakifuatilia kwa nyuma msafara wa waziri mkuu huyo mstaafu hadi kituo kikuu cha polisi wilaya ambako yalianza kufyatuliwa mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi ambao kwa wakati huo walikwishaanza kujazana nje ya kituo hicho kufuatilia kukamatwa kwake.
Wakiwa kituoni hapo,na baada ya kuhakikisha wananchi wamekimbia kuokoa maisha yao baadaye msafara wa waziri mkuu huyo mstaafu aliyekuwa ameongozana na Profesa Balegu,na Hamis Mgeja uliondoka kituoni hapo kuelekea makao makuu ya polisi mkoa wa Geita ukiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ambako hadi mtandao wa madukaonline unakwenda mitamboni bado viongozi hao wa chadema walikuwa ndani ya ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Geita wanakohojiwa.
Hata hivyo mbali na polisi kurusha mabomu ya machozi na kupiga risasi za moto kuwatawanya wananchi hao,waandishi wa habari wawili Robert na Maduka waliokuwa eneo hilo wakitekeleza majukumu yao ya kazi walikamatwa kisha kuanza kushushiwa kipigo na polisi huku Maduka akiumizwa sehemu za mgongoni wakati Robert akipigwa kwa mateke sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani,mgongoni na miguuni.
Maduka na Robert waliokolewa na OCD Kitumbo aliyefika eneo ambalo walikuwa wakipokea kipigo kisha kuwazuia askari wake wasiendelee kuwashambulia waandishi hao ambao kwa wakati huo walikwishakamatwa Tanganyika jeki wakilazimishwa kuingia kituoni ili wawekwe mahabusu.
Wakizungumza na MadukaOnline,waandishi hao walidai kuwa kitendo walichofanyiwa na polisi hao ni cha kinyama na hakikubaliki kwa vile kinavunja haki za binadamu ikizingatia kuwa walikuwa wakitekeleza majukumu yao bila kuvunja sheria za nchi.
"Kwa kweli nimeumizwa sana sehemu za mgongoni lakini pia kitendea kazi changu ambayo ni Kamera ilirushwa kwa minajili ya kuivunja lakini kutokana na ugumu wa kifaa changu hakikuweza kudhurika sasa najiuliza hivi hii ni haki na je Tanzania kuna uhuru wa vyombo vya habari maana kama mwandishi anavamiwa eneo lake la kazi kisha kupigwa bila sababu’’alisema Maduka.
Kwa upande wake Robert ambaye kwa sasa anachechemea kutokana na maumivu aliyoyapata kutokana na kipigop hicho alidai amesikitishwa na kitendo cha polisi kuvunja kamera yake ambayo amekuwa akiitumia kutekeleza majukumu yake na hajui iwapo jeshi hilo litamlipa au la.

Kwa mjibu wa waandishi hao wamedai wamepanga kuchukua PF3 kisha kufungua kesi mahakamani ili kudai haki zao kutokana na kitendo cha udhalilishaji walichofanyiwa.
Aidha klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita (GPC)mbali na kulaani kitendo hicho imeelekeza kwa waandishi waliokumbwa na madhila hayo kuhakikisha wanapata PF3 ili baadaye uongozi wa GPC umwandae wakili wake ambaye atasimamia kesi hiyo mahakamani.
‘’Nimesikitishwa na kitendo walichofanyiwa waandishi hao na nimeelekeza wahakikishe wanachukua PF3 ya matibabu ili tumwandae wakili wetu ambaye atasimamia kesi hiyo itakapofikishwa mahakamani lengo ni kuonyesha kukerwa na vitendo vya polisi vya kuwakamata na kuwapiga waandishi bila sababu wanapotekeleza wajibu wao wa kihabari’’alisema Mwenyekiti wa GPC Mkoa wa Geita Daniel Limbe.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita  Mponjili Mwabulambo amekanusha taarifa ya kukamatwa na kwamba walimzuhia kwaajili ya usalama na maswala mengi ambayo wamezungumzia ni jambo la ulinzi na kwamba walilenga katika swala la ulinzi wa jamii na usalama wa wao wenyewe.
“Kiswahili kizuri kwamba tulikuwa tumemzuhia hatukuwa tumemkatamata  isipokuwa tulikuwa tumemzuia ule msafara wake kwa ujumla nyuma ya kumzuhia kwake lilikuwa ni swala la usalama na ulinzi kwa ujumla”alisema Mwabulambo.
Powered by Blogger.