VYOMBO VYA HABARI NCHINI VYATAKIWA KUWA CHACHU YA MABADILIKO KUELEKEA MAENDELEO YA UCHUMI WA KATI.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape
Moses Nnauye akizungumza na uongozi na baadhi ya wafanyakazi wa Clouds Media
group wakati alipofanya ziara kujionea utendaji kazi wake na changamoto
wanazozipata katika kutekeleza majukumu yao.
|
Picha na Raymond Mushumbusi
Na Beatrice Lyimo
Serikali imevitaka vyombo vya habari nchini kuwa chachu ya mabadiliko katika
kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchumi wa kati.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye katika ziara yake kwa vyombo vya habari vya Clouds, Mlimani na Azam, ziara
inayolenga kuimarisha mahusiano yaliyopo baina ya Serikali na vyombo vya habari
nchini.
“Serikali ya Awamu ya Tano imejikita
katika ajenda mbalimbali ikiwemo kutoka katika hali ya uchumi tuliona nao sasa
kuelekea uchumi wa kati hivyo vyombo vya habari vinatakiwa kuwa mstari wa mbele
katika kuhakikisha suala hili linawafikia na kuleta uelewa kwa wananchi”alisema
Mhe. Nnauye.
Waziri Nape alisisitiza kuwa,
kumekuwa na mitazamo tofauti katika vichwa vya wananchi au jamii kwa ujumla
kuhusu suala zima la kuelekea uchumi wa kati, hivyo ni jukumu la vyombo vya
habari nchini kuweza kuwaelewesha nini maana halisi ya uchumi unaolengwa
kufikiwa.
“tumesikia ya kwamba uchumi wa nchi
umekuwa kwa asilimia saba, mwananchi wa kawaida hawezi kuwa na uelewa wa kujua
ni vipi uchumi wa nchi unakuwa, hivyo vyombo vya habari vina mchngo
mkubwa katika kuifanya jamii kuwa uelewa juu ya ukuaji wa uchumi” alisisitiza
waziri Nape.
Mbali na hayo Waziri Nape amesema
kuwa vyombo vya habari ni chanzo cha wananchi kuwa kitu kimoja katika kulinda
amani ya nchi na utamaduni uliopo, hivyo vina budi kuzidi kutunza utamaduni
uliopo pamoja na kuwafanya wananchi kupenda utamaduni wao.
Waziri Nape alisisitiza kuwa vyombo
vya habari viifanye jamii kwa ujumla kuwa na utamadumi hasa wa utamaduni wa
ulipaji wa kodi katika nyanja tofauti na kuwa wazalendo kwa maendeleo ya nchi.
“sisi kama wanahabari na vyombo vya
habari kwa ujumla tunatakiwa kutengeneza vijana ambao kwao kulipa kodi ni
fahari, vijana ambao kazi kwao ni heshima pamoja na kutengeneza vijana ambao
hujivunia uzalendo wa nchi yao"alisema Mhe. Nnauye
Hata hivyo Waziri Nape ameahidi
kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Serikali na vyombo vya habari nchini
katika nyanja tofauti ikiwemo utoaji wa habari muhimu za utekelezaji wa
Serikali katika kuleta maendeleo nchini.