VIGOGO WATATU WA TANESCO WASHUSHWA VYEO


Vigogo  watatu ambao ni wakurugenzi katika Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), makao makuu Dar es Salaam, wameshushwa vyeo huku mmoja akiamua kuacha kazi mwenyewe.

Hatua hiyo imekuja siku nne tangu Rais Dk. John Magufuli atengue uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Mramba alitenguliwa uteuzi wake siku chache baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.

Wakurugenzi hao wamesimamishwa jana kupisha uchunguzi, huku chanzo cha kusimamishwa kwao kikiwa hakijaelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya Tanesco ambayo ilithibitishwa na Kaimu Mkurugenzi mpya wa shirika hilo, Dk. Tito Mwinuka kwa simu jana, ilieleza kusimamishwa kwa vigogo hao ambao walikuwa wasaidizi wa karibu wa Mramba katika utendaji.

“Ni kweli wamesimamishwa, lakini kwa kuwa sikuwa ofisini ngoja niisome vizuri taarifa iliyopo mezani kisha niwatumie taarifa iliyokuwa sahihi kuhusiana na hilo.

“Hapa nilipo nipo ofisini na ofisa habari wangu (hakumtaja jina) tunaandaa taarifa ya pamoja, kwa maana kila mmoja anapiga simu kutaka taarifa, hivyo siwezi kuzitoa nusu nusu,’’ alisema Dk. Mwinuka.

Taarifa zinaeleza kwamba wakurugenzi watatu wameshushwa vyeo na kuhamishiwa katika Chuo cha Mafunzo cha Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika linaboresha ufanisi wake.

Walioshushwa vyeo ni pamoja na Declan Mhaiki ambaye alikuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji aliyekuwa anashughulikia usambazaji wa umeme.

Hata uamuzi huo unachukuliwa inaelezwa kuwa Mhaiki alikuwa kwenye msiba wa kaka yake mkoani Ruvuma, marehemu Kapteni Keenan Mhaiki.

Kapteni Mhaiki aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), alifariki dunia mapema wiki hii.

Wengine walioshushwa vyeo na kuhamishwa ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji na Huduma kwa Mteja, Mhandisi Sophia Mgonja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji Umeme, Nazir Kachwamba.

Wakati hao wakipigwa na panga hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu, Watson Mwakyusa, aliamua kuandika barua kuacha kazi mwenyewe.

Januari Mosi mwaka huu, Rais Magufuli alimteua Dk. Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, baada ya kumng’oa aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo, Mhandisi Mramba.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akiwa mjini Bukoba kwenye ibada ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli alisema amekerwa na kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kujitokeza hadharani na kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama uamuzi wa Serikali bila kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.

Kutokana na hali hiyo, alisema watendaji hao ni miongoni mwa majipu yanayostahili kutumbuliwa.

Hatua ya kutumbuliwa kwa Mramba ilikuja siku moja baada ya Ewura kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme.
Powered by Blogger.