MAJAMBAZI WATATU WAUAWA KATIKA MAPAMBANO NA POLISI DAR
Watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wameuawa katika tukio la
kurushiana risasi na polisi katika eneo la Mikocheni, karibu na Shule ya
Sekondari Feza jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon
Sirro watuhumiwa hao waliuawa jana asubuhi na majina yao bado
hayajafahamika.
Alisema marehemu hao ni waliohusika katika tukio la kupora zaidi ya Sh
milioni 26 katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la
Tazara, Dar es Salaam.
Hata hivyo, alipoulizwa ufafanuzi zaidi wa tukio hilo na je watuhumiwa
hao walikuwa na usafiri gani, Sirro alisema kuwa hizo ni taarifa za
awali na taarifa rasmi atazitoa leo.
Alisema kwamba miili ya marehemu, imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Taarifa zaidi zinadai kwamba watuhumiwa hao akiwemo mwanamke
aliyejisalimisha, ambaye ndiye alikuwa dereva wao, walikuwa na mpango wa
kufanya uvamizi katika maeneo hayo, ambapo pia baadhi yao walifanikiwa
kukimbia.
Lakini, Polisi haijathibitisha taarifa hizo na imeeleza kuwa itatoa taarifa zaidi leo.