Jitihada za
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan za kuiingiza
Tanzania katika mpango mkubwa wa Biashara kwenye bara la Asia, Mashariki ya
kati,Ulaya na Afrika umefanikiwa baada
ya Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi Saba kuingizwa katika mpango
unaojulikana kama China One Belt, One Road Stratergy.
Nchi nyingine
ambazo zimechanguliwa kuingizwa kwenye mpango huo ni Malaysia,Sri lanka, Nepal,
Bangladesh,Pakistan na Thailand.
Baada ya
Tanzania kuingizwa rasmi katika mpango huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambaye pia Mjumbe katika jopo la
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la kumuwezesha mwanamke kiuchumi akiwakilisha
nchi za ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika amekutana na Watendaji kutoka
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF),Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda
na Biashara (TCCIA) na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kuwaeleza kuhusu
muhimu wa Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo.
Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imepata uanachama wa mpango huo baada ya
kukutana na kufanya mazungumzo na Mfanyabiashara wa Madini na Vito kutoka China
Dkt Helen Lau kuhusu manufaa ya mpango huo na Makamu wa Rais alimwomba
Mfanyabiashara huyo kuisaidia Tanzania kuingia kwenye mpango huo China One
Belt, One Road Stratergy jambo ambalo limefanikiwa.
Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Mwezi Septemba mwaka 2016 ulifanyika mkutano
Guangdong nchini China kujadili maombi ya kujiunga na mpango huo ambapo Makamu
wa Rais alimwomba Dkt Helen kuiwakilisha Tanzania katika kuwasilisha maombi na
kwa bahati nzuri ombi la Tanzania lilikubaliwa na kupata uanachama katika
mpango huo mkubwa wa China One Belt, One Road.
Makamu wa Rais
amesema kuwa moja ya fursa zinazotolewa na Serikali ya China katika mpango huo
ni kila nchi Mwanachama kupewa vyumba vya ofisi katika jengo linaloitwa 21st
Century Maritime Silk Road Expo bila kulipa kodi ya pango kwa miaka Mitatu na
baadhi ya vyumba vya jengo hilo vitatumiwa na nchi husika kuonyesha na
kutangaza bidhaa zao.
Kufutia
Tanzania kuingizwa kwenye mpango, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza
watendaji wa sekta binafsi alikutana nao ikulu jijini Dar es Salaam wajipange
na kuweka mikakati ya namna ya kunufaika na mpango huo haraka iwezekanavyo.
Amesisitiza
kuwa mpango huo wa China One Belt, One Road Stratergy uliobuniwa na serikali ya
China kwa dhamira ya kuzikutanisha Jumuiya za Wafanyabiashara za Mashariki mwa bara Asia, Mashariki ya kati,
Ulaya na Afrika kwa ajili ya kubadilishana mawazo,kuonesha njia na kupeana ushauri
wa jinsi ya kukuza biashara kati ya nchi wanachama wa mpango huo kwa lengo la
kuiwezesha sekta ya biashara kuchangia nyema kwenye uchumi wa mataifa yao.
Makamu wa Rais
Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania baada ya kuingia kwenye mpango huo
itanufaika na fedha za mfuko kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ambazo
zinatolewa kwa nchi zilizojiunga na mpango huo.
Kwa upande
wake, Mweyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania Godfrey Simbeye na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar
Taufik Turki wamemuahidi Makamu wa Rais kuwa watatumia fursa hiyo ipasavyo ili
kukuza biashara kati ya Tanzaniana Nchi wanachama wa mpango huo.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es Salaam
6-Jan-2017. |