Picha: WATU 14 WAFUKIWA NA KIFUSI CHA UDONGO WAKICHIMBA MADINI MKOANI GEITA


WATU kumi na nne akiwemo raia wa China wamefukiwa na udongo usiku wa kuamkia leo majira ya saa saba usiku (7:00) wakiwa wanaendelea na majukumu yao ya uchimbaji madini  kwenye kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya RZ iliyopo kijiji cha Nyarugusu  mkoa wa Geita.

Inaelezwa kuwa udongo umeporomoka kutokana na mgodi kuchimbwa zamani na Wajerumani hivyo kusababisha baadhi ya maeneo hayo kuwa na nyufa na vyuma kushindwa kushikilia udongo wa juu hali ambayo imesababisha kuzidiwa na hatimaye kuporomoka.

Kamisha msaidizi wa madini kanda ya ziwa victoria Mhandisi Yahaya Samamba  amesema jitihada zilizofanyika ni kuwasiliana na migodi iliyopo karibu na eneo hilo pia wameomba msaada kutoka Kahama na kwenye mgodi wa GGM kupatiwa vifaa vya uokoaji ili zoezi hilo liweze kufanikiwa.

“Jitihada ambazo tumezifanya hadi sasa tumeomba msaada Kahama na kwenye mgodi wa Geita,kupatiwa vifaa ambavyo vitasaidia kwa wepesi zoezi hili la uokoaji ingawa tumeshapata vifaa vingine kutoka kwenye mgodi wa Busolwa”,alisema Samamba.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita Elisa Mugisha amesema eneo la chini ambalo limefukiwa na udongo ndiyo ambalo sasa wanaendelea kulitanua ili sehemu hiyo iwe kubwa watu waweze kupita.

“Eneo lote lile la chini limefukiwa na udongo lakini kule chini kunaonekana kuna sehemu za kwenda pembeni ingawa limefukiwa lakini chini kuna uimara kuna uwezekano kule chini wale watu wapo hai na wamepelekewa mipira ya hewa na kazi inayofanyika ni kutanua eneo ambalo litasaidia kuwatoa watu hao",amesema.
Mwanasheria na msemaji wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya RZ  Frances Kiganga ameelezea kuwa chanzo kikubwa ni mashimo ya zamani kwani udongo unapotikisika umekuwa ukisababisha baadhi ya nyufa kuendelea kupata shida.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga amewataka wanaosimamia zoezi la uokoaji kuongeza nguvu ya uokoaji.
Tazama picha hapa chini

Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akiambatana na msemaji wa mgodi huo Frances Kiganga pamoja na kamanda wa zimamoto,Elisa Mugisha wakielekea kwenye eneo ambalo shimo limejifukia-Picha zote kwa hisani ya Madukaonline blog
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita Elisa Mugisha akielezea namna wanavyoendelea na jitihada za kuokoa 
Kamisha msaidizi wa madini kanda ya ziwa victoria Mhandisi Yahaya Samamba akifafanua jambo
Mmoja kati ya wafanyakazi kwenye mgodi huo akielezea hali ilivyotokea na jinsi shimo lilivyojifukia
Eneo la shimo  hilo ,uokoaji ukiendelea
Jitihada za uokoaji zikiendelea
Baadhi ya waokoaji wakiwa eneo la tukio
Shughuli za uokoaji zikiendelea 
Mwanasheria na msemaji wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya RZ Frances Kiganga ,akielezea chanzo cha mgodi huo kujifunika.
Chanzo-Madukaonline blog
Powered by Blogger.