MTOTO AFARIKI BAADA YA KUTUPWA KWENYE CHOO CHA KANISA LA AICT KITANGIRI SHINYANGA
Mtoto mwenye umri wa siku moja mwenye jinsia ya kiume amefariki dunia
baada ya kutupwa na mtu asiyefahamika katika tundu la choo la Kanisa
la African Inland Church Tanzania (AICT) lililopo Kitangiri manispaa
ya Shinyanga.
Tukio hilo limetokea Januari 20,2017 saa 11 jioni ambapo waumini wa
kanisa hilo walisikia sauti ya mtoto ikitokea katika tundu la choo cha
kanisa.
Akisimulia kuhusu tukio hilo Mwenyekiti wa mtaa wa Kitangiri Habiba
Jumanne alisema alipigiwa simu na baadhi ya waumini wa kanisa hilo
kuwa kuna sauti ya mtoto mchanga inasikika kutoka ndani ya tundu la
choo.
“Tulifanya jitihada za kuvunja choo na kumtoa mtoto akiwa hai
tukamkimbiza hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga cha kusikitisha leo
asubuhi Januari 21,2017 tumekwenda kuona hali ya mtoto,daktari
ametueleza kuwa mtoto amefariki dunia”,alisema Jumanne.
Jumanne alisema baada ya kuvunja choo hicho na kumtoa mwili wake ulikuwa
umetapakaa kinyesi hivyo walimuogesha maji ya baridi huenda maji
hayo yamechangia kupatwa na baridi kali na kusababisha kupoteza uhai
wake.
Mwenyekiti huyo alisema mpaka sasa mtu aliyefanya kitendo hicho
hajajulikana na wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini kama kuna
mkazi wa eneo hilo ndiyo kahusika na kwamba tayari wameomba kibali
kutoka cha polisi ili kwenda kuzika mwili wa mtoto huyo kwa kushirikiana
na kanisa la AICT.
Hata hivyo alitoa wito kwa jamii kuacha mara moja vitendo vya kinyama na
kama wanaona maisha magumu kulea watoto wawapeleke kwenye mashirika au
taasisi za kulea watoto wakapate kukua kuliko kutenda unyama wa mauaji
Hata hivyo Mzee wa kanisa la AICT David Madata alisema wakati
akifundisha watoto somo la Injili kanisani hapo alimuona mwanamke mmoja
aliyekuwa amelala karibu na choo hicho lakini hawakumdhania kama
atafanya unyama huo baada ya muda aliondoka kusikojulikana na kuanza
kusikia sauti ya mtoto mchanga kwa waliokuwa wakienda chooni hivyo
waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi na serikali ya mtaa.
Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga SSP Elias Mwita
alisema mtoto huyo alitupwa kwenye tundu la choo la kanisa la AICT na
mtu ambaye hajafahamika na wanaendelea na uchunguzi kumbaini aliyehusika
na kitendo hicho.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog