Frank Mvungi
Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa
kuna utoshelevu wa dawa kwa asilimia 86 kinyume na taarifa za upotoshaji
zinazotolewa na baadhi ya watu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Leo
Jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mkuu wa Bohari kuu ya Dawa (MSD) Bw.
Laurean Rugambwa amesema kuwa Serikali
ya awamu ya tano imetenga bajeti yakutosha kukidhi mahitaji ya dawa hapa nchini
ambapo kufikia machi 2017 upatikanaji wa Dawa utafikia asilimia 90.
“ Serikali imetenga bilioni 250 katika
bajeti ya mwaka huu na Kila mwezi Serikali inatoa zaidi ya bilioni 20 ajili ya ununuzi wa dawa hali iliyosaidia
kuondoa tataizo la dawa hapa nchini kwa sasa”
Akifafanua Rugambwa amesema kwa sasa
fedha sio tatizo kwa Bohari ya dawa kutokana na hatua za makusudi
zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano katika kuhakikisha kuwa Watanzania
wanapata huduma bora za afya ikiwemo upatikanaji wa dawa.
Moja ya mikakati iliyochukuliwa na
Serikali katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa ni kuboresha matumizi ya mfumo wa msimbo pau
(Barcode) hali itakayosaidia kuongeza ufanisi katika upokeaji,utunzaji na
usambazaji wa dawa na vifaa tiba.
Mikakati mingine ni kuanziasha mpango wa
huduma maalum kwa wateja wakubwa ambao ni Hosipitali ya Taifa Muhimbili,MOI,
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitai ya Bugando,Hosipitali ya
Kibongoto,Hospitali ya Mirembe,Hospitali ya Amani, Hospitali ya Temeke,
Mwanenyemala,Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya,KCMC, Hosipitali ya Benjamin
Mkapa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Pia kununua dawa moja kwa moja kutoka
kwa wazalishaji na kuanzisha mchakoto wa ujenzi wa viwanda vya kuzalisha dawa
na vifaa tiba nchini ili kupunguza gharama.
Katika kipindi cha mwaka 2016 MSD
imefungua maduka ya dawa sehemu mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwezesha
Hospitali ambazo ndio wateja wakubwa wa MSD,Maduka ambayo mpaka sasa
yameshafunguliwa ni pamoja na lile lililopo katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili,Sekou Toure Mwanza,Hospitali ya rufaa Mbeya,Mount Meru Hospitali
,Chato Halmashauri ya Mji wa Geita na Ruangwa Mkoani Lindi. |