MAKAMU WA RAIS TANZANIA ATUMA SALAMU ZA PONGEZI KWA MKUU WA MKOA WA GEITA KUOKOA WACHIMBAJI 15 WALIOFUKIWA UDONGO MGODINI
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
amemtumia salamu za pole na pongezi Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali
Mstaafu Ezekiel Kyunga kwa kazi nzuri na kubwa waliyoifanya ya kuwaokoa
wachimbaji wadogo 15 waliofukiwa na maporomoko ya udongo kwenye Mgodi wa
Dhahabu wa RZU uliopo katika Kijiji cha Nyarugusu, wilaya ya Geita
katika mkoa wa Geita.
Tukio hilo la kufukiwa wachimbaji hao wadogo 15 wakiwemo Watanzania 14
na raia Mmoja wa China lilitokea usiku wa Tarehe 26 Januari mwaka 2016.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema amepokea kwa furaha taarifa za kuokolewa kwa wachimbaji
hao wadogo na amesifu na kupongeza jitihada za kuwaokoa wachimbaji hao
zilizofanywa na Serikali ya Mkoa wa Geita, Jumuiya ya Wachimbaji Wadogo
wa mkoa wa Geita, Wamiliki wa Migodi ya Dhahabu na wananchi kwa ujumla
kwa kutoa vifaa mbalimbali vya uokoaji jitihada ambazo zimepelekea
kuokolewa kwa wachimbaji hao wakiwa hai.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa “jitihada ,Umoja na Mshikamano
ulioonyeshwa na makundi mbalimbali katika kuwaokoa ndugu zetu
waliofukiwa na maporomoko ya Udongo wakiwa kazini huko Geita ni mfano
mzuri na wakuigwa na wananchi na taasisi nyingine nchini katika
kujitolea kwa hali na mali hasa vifaa vya uokoaji kwa ajili ya kusaidia
watu wanaopatwa na majanga ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea kama
walivyofanya ndugu zetu wa mkoa wa Geita nawapongeza Sana”.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wamiliki wa migodi kote
nchini wahakikishe wanafanya kazi zao za uchimbaji wa madini kwa
kuzingatia kanuni,taratibu na sheria kama hatua ya kuepuka madhara
yanayoweza kutokea wakiwa wanafanya shughuli zao za uchimbaji wa madini.
Kupitia kwako Mkuu wa mkoa wa Geita napenda kutuma salamu za pole kwa
ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kutokea kwa tukio hilo na nawaombea
kwa Mwenyezi Mungu wachimbaji hao ambao kwa sasa wanapatiwa matibabu
Katika Hospitali ya Serikali ya mkoa wa GEITA matibabu mema ili waweze
kupona haraka na kurejea kwenye kazi zao za kujitafutia riziki.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe
Samia Suluhu Hassan ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha
Kudhibiti Maafa nchini, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya
Mambo ya Ndani kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Ofisi ya Mkuu wa
mkoa wa Geita na kupekelea kuchukuliwa hatua za haraka katika
kushughulikia ajali hiyo.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dar es Salaam
29-Jan-2017