BULEMBO AMTAKA LOWASSA AACHANE NA SIASA ILI KUFAIDI UZEE WAKE VIZURI
Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo
amemshangaa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwa kuendelea
kung’ang’ania siasa hadi sasa hivi, badala yake anastahili kukaa kimya
kula maisha ili afaidi uzee wake vizuri.
Bulembo aliyasema hayo wakati akifunga kampeni za udiwani Kata ya
Mateves iliyopo Wilaya ya Arusha juzi, ambako walitarajiwa kumchagua
diwani wao katika uchaguzi mdogo. Mbunge huyo mteule wa kuteuliwa,
alisema anashangaa Lowassa kung’ang’ania madaraka, badala yake
anastahili kula maisha ili kufaidi uzee wake vizuri.
Alisema wapinzani wataruhusiwa kutumia barabara, maji, shule na vinginevyo, lakini kwenda Ikulu haiwezekani.
Aidha, Bulembo alilaani kitendo cha wafuasi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kuingilia msafara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
uliokuwa ukielekea Uwanja wa Ngorbob Sokoni kwa ajili ya kufunga kampeni
za chama hicho.
Alisema wafuasi wa CCM ni wastaarabu na wavumilivu, hawakufanya fujo,
bali waliwapita kwa mbele na kuelekea kwenye mkutano wa kufunga kampeni.
Mgombea Udiwani wa Kata ya Mateves, Julius Saing’ore maarufu kwa jina la
Sovoyo na mgombea uenyekiti wa serikali ya kijiji, Mohamed Nassoro
maarufu kwa jina la Arsenal, waliomba kura kwa wananchi hao ili walete
maendeleo.
Mgombea udiwani Saing’ore aliwasihi wananchi wa kata hiyo, kumpa kura
ili waliokwenda mahakamani kudai uchaguzi uliokuwa na kasoro wajue kuwa
CCM ndio yenyewe.
Awali, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shabani Mdoe
alisema wananchi wana imani kubwa na chama hicho na hawataki porojo,
bali wanataka maendeleo.
Alisisitiza kuwa awali alipokuwa madarakani aliyekuwa diwani wa CCM
kabla ya kutenguliwa na mahakama mwaka jana, Saing’ore maarufu kwa jina
la Sovoyo, alifanya kazi mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuhakikisha
wananchi wanapata maji safi na salama.
Alisema diwani huyo ambaye sasa anagombea tena, alikaa madarakani kwa
siku 63 kama Diwani wa Kata ya Mateves kwenye Halmashauri ya Wilaya ya
Arusha Vijiji (Arusha DC) hivyo kurudi kwake kama diwani kutawezesha
wananchi kupata maendeleo.