Ajitia kitanzi kwa kukatazwa kumrithi shemejie Rorya





  Mkazi  wa kijiji cha Muharango kata ya Nyamagaro wilayani hapa mkoani Mara amefariki dunia kwa kujinyonga kwa kamba ya katani hadi kufa kwa  madai ya mama yake mzazi kumtaka amwache shemeji yake aliyemrithi.

 Lukas Jenge (24) alijikatisha maisha januari 21 baada ya mama yake kumtaka aachane na shemiji yake aliyekuwa amekita mizizi ya penzi kwa kipindi kirefu baada ya kaka yake kufariki.

Kitendo hicho cha mara kwa mara cha mama yake kumtaka aachane na shemeji yake kilimfanya achukue maamuzi hayo magumu kwa madai ya kumwachia mama yake wakwe wawili kwani tayari alikuwa amekiwshi kuoa.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Jumanne Mkirya alisema kijana huyo alichukua uamuzi huo majira ya saa tano usiku wa januari 21, kwa kujita kitanzi na kufariki dunia.

“Nilipigiwa simu usiku saa 10:00kuwa mtu amefariki kwa kujinyonga na nilipofika nilimkuta amekwisha kufa ikabidi tukate kamba na kutoa taarifa polisi ambao walifika na kumchukua kwa uchunguzi zaidi,”alisema Mkirya.

Mkirya  aliongeza kuwa kijiji hicho kimekuwa na matukio mengi ya wananchi kujinyonga na kusema inahitajika elimu kwa wananchi hao ilikuondoa dhana ambayo wemejijengea ya kuwa njia ya kutatua mataizo yao ni kujinyonga na kunywa sumu.

“Matukio ni mengi wengine wanapona na kuendelea kuishi,lakini tunaomba wanapobainika kunusurika wachukuliwe hatua kwa kitendo kile, lakini pia wazazi tusiingilie maamuzi ya watoto kwani tayari walishaamua na kufikia pale,”alisema Mkirya.

Wakati huo huo katika kitongoji cha Nyangabo kijiji cha Nyang’ombe, kijana aliefahamika kwa jina la Babu Greeni (24) alifariki dunia kwa kunywa sumu.

 Mjomba na marehemu huyo, Mourice Kayaka alidai kuwa baada ya kufariki mama yake, marehemu aliondoka kwenda kumtafuta baba yake mzazi  hadi mauti ilipomkuta.

“Nilikuwa nilishamsahau maana aliondoka tangu akiwa mdogo hata sijui kama amefariki wala kama amezikwa, lakini mama yake alikuwa dada yangu baada ya kuolewa na mume mwingine,kijana huyo aliondoka nyumbani kwenda kumtafuta baba yake tangu hapo hatukuwahi kumwona,”alisema Kayaka.

Kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Tarime/ Rorya Andrew Satta alithibitisha kuwapo kwa matukio hayo na kuitaka jamii kuachana na tabia ya kujiondolea uhai kwani siyo suluhisho sahihi la matazo yao.

“Haya ni mambo ya kijamii wazazi wanaweza kuwa chanzo, mila na desturi zinaweza kuwa chanzo  cha matatizo haya, lakini pia jamii tushiriki kuiasana kuacha kujitoa roho na pia wazazi kusimamia mambo ya msingi katika jamii kwa ujumla,”alisema Satta.


Powered by Blogger.