SUALA LA UKEKETAJI MKOANI MARA BADO NI PASUA KICHWA.
Baadhi ya wasichana wakitoka kukeketwa
wilayani Tarime mkoani Mara, kumbuka mwezi Disemba, kila baada ya miaka
miwili, ni msimu wa ukeketaji na tohara kwa baadhi ya Koo za Wakurya.
#BMGHabari
Pamoja na
juhudi za Serikali, Wanaharakati na Watetezi wa haki za binadamu
(Wanawake na Wasichana) katika kuhakikisha kwamba suala la ukeketaji
linatokomezwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Mara na
Arusha, bado suala hilo ni pasua kichwa kwani linafanyika, iwe kwa uwazi
ama usiri.
Mtandao wa
Binagi Media Group umeshuhudia baadhi ya wakazi wa wilaya ya Tarime
wakisherehekea msimu huu wa ukeketaji (Mwezi Disemba kwa baadhi ya koo,
ikiwemo Watimbaru) ambapo wasichana wadogo wanafanyiwa ukeketaji.
Shamra shamra
zinafanyika hadharani licha ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga,
kuonya kwamba yeyote atakayebainika kujihusisha na ukeketaji
atachukuliwa hatua za kisheria.
Baadhi huamini
kwamba msichana akikeketwa huleta heshima kwake na kwa familia na huwa
tayari kwa ajili ya kuolewa na hivyo kuwapatia wazazi mahari (ng'ombe).
Hatua hii husababisha baadhi ya mabinti kukosa fursa ya kuhitimu masomo
yako na kujikuta wakiolewa, Aidha kwa kupenda ama kulazimishwa na
wazazi/walezi wao. Suala la unyanyapaa miongoni mwa wasichana
waliokeketwa na ambayo hawajakeketwa ni jambo ambalo pia huongeza
msukumo wa wasichana kutaka kukeketwa. Mbaya zaidi, unyanyapaa huo
huenda hadi kwa baadhi ya wanaume kukataa kuwaoa wale ambao
hawajakeketwa na hivyo kusababisha ugumu wa kutokomeza suala hilo.
Tayari Ngariba
mmoja aitwaye Angelina ppCharles (50) amehukumiwa kifungo cha miaka
miwili gerezaji kwa kosa la kumfanyia ukeketaji mmoja wa wasichana
wilayani humo huku wengine wawili wakidaiwa kukabiliwa na kesi ya aina
hiyo. Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya
ya Tarime, Mhe.Martha Mpaze.
Wakati hayo
yakiendelea, zipo kauli mbalimbali wilayani Tarime kwamba hivi sasa
wasichana hawakeketwi kama zamani bali wakifika eneo la tukio hupakwa
unga kwenye uso na maumbile yao na kufanyiwa matambiko ya kimila na
shughuli huishia hapo na kinachofuata ni shamra shamra za kucheza ngoma
ya ritungu na kurejea nyumbani.
Hata hivyo
utafiti uliofanywa mwishoni mwa mwaka jana na Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania, TAMWA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa
Mataifa linalojihusisha na idadi ya watu duniani, UNFPA, kwenye mikoa 13
nchini ikiwemo Mara, umebaini kwamba katika maeneo mengi nchini,
wanajamii wanazo mbinu mpya za kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya
kukumbatia mila potofu ikiwemo ukeketaji. Utafiti huo ulibaini kuwa,
suala la kuwapaka unga usoni wasichana wilayani Tarime ni kuuficha tu
ukweli kwamba wasichana hao hawakeketwi wakati ukweli ni kwamba
hukeketwa.
Itoshe tu
kusema kwamba, elimu zaidi inahitajika ili kuwanusuru wasichana
wanaotoka kwenye makabila yanayojihusisha na ukeketaji kwani madhara
yake ni makubwa ikiwemo kupoteza damu nyingi, kupata madhara kabla na
baada ya kujifungua, kupoteza uwezo wa kufurahia tendo la ndoa,
uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa ikiwemo Virus vya Ukimwi na
wakati mwingine kupoteza maisha.
Inaelezwa kwamba msichana anayekeketwa
hulipia kiasi cha shilingi elfu 35 hadi 40 ambapo wazee wa kimila
hugawana pesa hiyo na mangariba hivyo inawezekana suala hili linakuwa na
ugumu kutokomezwa maana ni sehemu ya ujira kwa wazee na mangariba hao.
Inadhaniwa kwamba zaidi ya wasichana
3,000 kwa Koo moja ya kabila la Wakurya hukeketwa kwa kila msimu. Kabila
la Wakurya lina Koo 13.
Wakazi wa Wilaya ya Tarime wanasema,
msukumo wa ukeketaji umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka
ya nyuma. Wanasema suala la elimu juu ya madhara ya ukeketaji pamoja na
mwingiliano wa makabila mbalimbali ya ndani na nje ya mkoa wa Mara,
umesaidia japo kwa kiasi kidogo kupunguza ari ya ukeketaji.
Kataa Ukeketaji,
haina umuhimu kufurahia mila na tamaduni zenye athari katika jamii.
Vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuwakama na kuwafungulia
mashtaka.
Wakati haya yanaendelea, zaidi ya
wasichana 250 kutoka maeneo mbalimbali mkoani Mara na Arusha,
wamehifadhiwa katika kituo cha kuwahifadhi wasichana waliokimbia
ukeketaji cha Masanga kilichopo wilayani Tarime.
BMG inaamini kwamba, Imani humalizwa kwa
Imani. Suala la Ukeketaji ni Imani hivyo itolewe elimu yenye uhusiano
wa kiimani ikiwemo maandiko matakatifu (dini) hatua ambayo itasaidia
kuwanusuru wasichana wengi na suala hilo la ukeketaji.