RAIS MAGUFULI AGOMA SHULE KUITWA JINA LAKE
Rais John Magufuli amekataa shule ya msingi iliyojengwa hivi karibuni eneo la Bunju, Wilaya ya Kinondoni kuitwa kwa jina lake badala yake ameagiza iitwe kwa jina la Mkuu wa wilaya hiyo, Ally Hapi.
Taarifa
ya badiliko la jina haikutolewa na Idara ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Ikulu kama ilivyozoeleka bali na mkuu wa wilaya hiyo wakati wa hafla ya
kukabidhi vifaa mbalimbali vya usafi kwa uongozi wa shule hiyo.
“Shule
hii imejengwa kwa fedha zilizopatikana baada ya Serikali Kuu kubana
matumizi. Tukaamua iitwe John Magufuli lakini yeye akatoa agizo shule
ipewe jina la mkuu wa wilaya sina budi kukubaliana na hilo,”alisema Hapi.
Shule
hiyo mpya iliyopo Bunju jijini imejengwa kwa lengo la kupunguza
msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Bunju A ambayo ilikuwa na
wanafunzi 3,224.
Mwalimu
mkuu wa shule hiyo mpya, Ali Mwakapalila alisema ingawa inatarajiwa
kuanza kupokea wanafunzi Januari 9 mwakani inakabiliwa na changamoto
mbalimbali.
“Hakuna umeme wala maji, hii inaweza kuleta madhara kwa wanafunzi hasa linapokuja suala la matumizi ya vyoo,” alisema.
Baada
ya hafla hiyo, Hapi alikwenda kwenye kiwanda cha saruji cha Twiga
Cement ambako alipokea msaada wa mifuko 600 ya saruji kwa ajili ya
kufanikisha ujenzi wa madarasa na majengo mengine.
Akipokea
msaada huo, Hapi alisema msaada kutoka Twiga Cement unaunga mkono
juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoipa sekta ya elimu kipaumbele
ili kuhakikisha inatolewa katika mazingira bora.
“Msaada
huu umekuja muda muafaka. Tumeshajenga shule ila tunataka kuongeza
madarasa, maabara, ofisi ya elimu na kuzungushia uzio ili watoto wawe
katika mazingira salama. Lengo ni kuifanya shule hii iwe ya kisasa na
itakuwa mfano kwa shule zote za Wilaya ya Kinondoni,”alieleza.
Pia, Hapi alisema wilaya hiyo ipo kwenye mipango ya kujenga maktaba ya kisasa kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya saruji.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Twiga Cement, Alfonso Velez alisema kuchangia katika
shughuli za kijamii ni moja ya mambo ambayo wamekuwa wakiyapa kipaumbele
zaidi.
“Kushiriki shughuli za maendeleo katika jamii ni jambo ambalo tunalipenda zaidi. Yalipo maendeleo Twiga Cement ipo pia,” alisema Velez.