Picha: WAZIRI MKUU ATEMBELEA GEREZA LA UKONGA KUKAGUA ENEO LA UJENZI WA MAKAZI YA ASKARI WA MAGEREZA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea gereza la Ukonga jijini Dar es
Salaam na kukagua eneo la ujenzi wa makazi ya askari wa Magereza
unaotarajiwa kuanza baada ya wiki tatu zijazo.
Akizungumza na askari wa magereza kabla ya kufanya ukaguzi huo jana
Jumamosi, Desemba 24, 2016 Waziri Mkuu alisema ziara aliyoifanya , ni
ufuatiliaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliyoitoa
wakati alipoenda kukagua gereza hilo.
Novemba 29, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara kwenye gereza hilo
na kupokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo
zipatazo 9,500 na akaagiza zitafutwe sh. bilioni 10 haraka ili kupunguza
tatizo hilo.
Akizungumzia kuhusu ujenzi huo, Waziri Mkuu alisema amefarijika kukuta
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wako eneo la kazi na wameanza kusafisha
eneo hilo.
“Nimefarijika kukuta TBA wako kazini na nimeelezwa hatua inayofuata ni
upimaji wa sampuli za udongo kabla hawajaanza kujenga msingi.
Nawapongeza TBA kwa kazi nzuri wanazofanya za ujenzi wa nyumba zenye
viwango na kwa haraka kama tulivyoona kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
na nyumba za Magomeni Kota,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua mchango uliofanywa na Serikali ya
awamu ya nne katika suala la makazi ya askari kama vile wa Jeshi la
Wananchi (JWTZ) na Jeshi la Polisi.
“Nia ya Serikali ni kuhakikisha makamanda wote wanapata nyumba nzuri ili
waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa wakiwa na uhakika familia
zao zimetulia kwenye makazi bora”.
Alisema katika ziara alizozifanya kwenye mikoa mbalimbali, alitembelea
magereza ya Isanga, Msalato (Dodoma), Lindi, Singida na Keko (Dar es
Salaam) alikuta nyumba za askari hazina viwango na kama zipo zimechakaa
sana.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa nyumba hizo, Kaimu Kamishna
Jenerali wa Magereza, Juma Malewa alisema wanamshukuru Mheshimiwa Rais
kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa makazi ya askari na kwamba jeshi hilo
litafanya kazi zote zisizo za kitaalamu ili kuokoa fedha za Serikali na
badala ya kulipwa watu binafsi, fedha hizo zitatumika kuongeza nyumba
zaidi.
“Tumekubaliana na TBA kazi zote zisizohitaji utalaamu kama kufyatua
matofali, kubeba mizigo au kufyeka zitafanywa na askari wetu pamoja na
wafungwa ili tuokoe gharama zote hizo na badala ya kulipa watu binafsi,
fedha hizo zitumike kujenga nyumba nyingine 80,” alisema huku
akishangiliwa.
Alisema wamejipanga kufanya kazi hizo kwa saa 24 kila siku ili kuokoa
muda ambao TBA walikuwa wameuweka wa kukamilisha ujenzi ndani ya miezi
minane.
Alisema wako tayari kuanzisha kambi za ujenzi kwa kutumia wafungwa na
askari ili wafanye kazi zisizohitaji utaalamu na fedha zitakazopatikana,
badala ya kuwalipa watu binafsi zitumike kujenga nyumba zaidi za
askari.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Bw. Baltazar Kimangano
alisema wanataraji kuanza ujenzi ndani ya wiki tatu baada ya kupokea
matokeo ya uchunguzi wa sampuli za udongo kutoka taasisi ya BICO ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema wanataraji kujenga majengo (block) manne ya ghorofa sita kila
moja ambayo kwa ujumla yatakuwa na nyumba 240 zenye ukubwa wa vyumba
viwili vya kulala. Pia watajenga majengo (block) mengine mawili ya
ghorofa sita kila moja ambayo yatakuwa na nyumba 80 zenye ukubwa wa
vyumba vitatu vya kulala.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua gwaride lililoandaliwa na Jeshi la
Magereza wakati alipowasili kwenye gereza la Ukonga jijini Dar es salaam
kukagua maadlizi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari Magereza
Desemba 24, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea heshima kutoka kwa gwaride
lililoandaliwa na Jeshi la Magereza wakati alipowasili kwenye gereza la
Ukonga jijini Dar es salaam kukagua maadlizi ya ujenzi wa nyumba za
makazi ya Askari Magereza Desemba 24, 2016.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza
wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokwenda kwenye Gereza la Ukonga
kukagua maandalizi ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari Magereza
Desemba 24, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maadalizi ya eneo la ujezi wa
nyumba za askari magereza katika gereza la Ukonga jijini Dar es salaam
Desemba 24, 2016. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani,
Mhandisi Hamad Masauni na kushoto kwake ni Kaimu Kamishina Jenerali wa
Magereza, Dkt. Juma Ali Malewa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa
Jeshi la Magereza baada ya kukagua maandalizi ya eneo zitakapojengwa
nyumba za makazi za Askari magereza katika gereza la Ukonga jijini Dar
es salaam Desemba 24, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU