HALI YA MAMBO NCHINI CONGO YAZIDI KUWA TETE.
Hali ya mambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo imezidi kuwa tete huku makumi ya watu wakiuawa katika
maandamano na mapigano ya kikabila.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch
limesema idadi ya watu waliouawa hadi sasa katika maandamano
yalioyaoanza Jumatatu dhidi ya Rais Joseph Kabila baada ya muhula wake
wa uongozi kumalizika imeongezeka na kufikia watu 34.
Ida Sawyer, Mkurugenzi wa eneo la Afrika ya Kati wa Human Rights
Watch amesema, watu 19 wameuawa na maafisa usalama katika maandamano
mjini Kinshasa, watano mjini Lubumbashi na sita katika miji bandari ya
Goma na Matadi, magharibi mwa nchi. Hata hivyo serikali ya Kinshasa
imesema ni watu 22 pekee waliouawa katika makabaliano kati ya
waandamanaji na maafisa usalama na kwamba polisi kadhaa pia wameuawa.
Hii ni katika hali ambayo, watu wengine 18 akiwemo afisa wa
polisi wameuawa leo Alkhamisi katika mapigano yaliyotokea kati ya
makundi mawili hasimu ya waasi katika mkoa wa Mongala, kaskazini
magharibi mwa nchi.
Captain Guillaume Djike, msemaji wa polisi katika mkoa huo amesema
baadhi wameuawa kwa kufyatuliwa risasi na wengine kwa kukatwa kwa
mapanga, baada ya kujiri mapigano kati ya kundi la waasi la Mai Mai
Mazembe wa kabila la Nande na wapiganaji wa Nyatura wa kabila la Hutu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka Ban Ki-moon ametoa wito
kwa pande zote zinazohusika katika mgogoro wa kisiasa huko Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kutatua mgogoro huo kwa njia za amani.
Upinzani katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo umewataka wananchi kutomtambua tena Joseph Kabila
kama rais wa nchi hiyo na umewahimiza kuonesha upinzani wao dhidi ya
Kabila kwa njia ya amani.