WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa
ufafanuzi kwamba haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa
kujiunga na vyuo vikuu badala yake walichokataza ni wanafunzi waliofeli
kidato cha nne na cha sita kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti
vyenye sifa.
Aidha, imesema kwa waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni
wajibu wa waajiri wao kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na
kutumia fursa hiyo kufanya mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo jana
Dar es Salaam kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea mitandaoni
kwamba serikali imepiga marufuku watu wenye Stashahada kujiunga na vyuo
vikuu badala yake watakaoingia ni wenye sifa za kidato cha sita.
Manyanya alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha
wanakuwa na sifa za shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya
kufanya mitihani hiyo waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia
wataweza kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kusoma vyuo vikuu.
“Ni vitu tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu
anakaa nafasi kwa sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki
utafanyika kwa vyeti na wanaofanya hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu
Waziri.
Alisema kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo zilikuwa
hazitakiwi kwa wakati huo ni batili zitafutwa na kwa watakaoingia kwa
sasa vyuoni kwa kutumia njia zisizo rasmi na kubainika hata ikifika
mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa taarifa tayari wanayo.
“Kilichoongelewa siku ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha sita
waliofeli kuingia kwenye ‘foundation course’ na diploma haikutajwa pale
kwa kuwa haikuulizwa na hakuna kauli iliyotajwa pale kukataza watu wa
diploma kwenda chuo kikuu,” alieleza Manyanya akirejea kauli ya Waziri
wake, Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni katika mahafali ya Chuo
Kikuu Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.
Profesa Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.
“Nami ningependa nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei mtu
sifa. Kama sifa ya kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha sita,
kama amefeli Baraza la Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa nini
anakwepa kule? Kwa nini? Kwa nini tunataka tuendeleze uchochoro,”
alieleza Waziri Ndalichako.
Naibu Waziri alisema kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo njia
ya moja kwa moja na njia ya mbadala ya kuwa na vyeti vinavyotambulika na
kinasimamiwa na mamlaka husika ambayo ni Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi (NACTE) na wawe na ufaulu mzuri.
“Tanzania imejiwekea mifumo yake ya elimu ambayo inaendana na ngazi za
kimataifa katika utoaji wa elimu na hapo awali tulikusudia kuhakikisha
elimu inatolewa kwa watu wengi zaidi na hizo fursa zinawafikia wadau
wote katika ngazi mbalimbali kwa kupanua elimu ya msingi hadi vyuo
vikuu,” alieleza Naibu Waziri.
Alisema walitambua kuna wadau mbalimbali walitamani kusoma vyuo vikuu,
lakini hawapati hiyo fursa na ndiyo wakaanzisha mfumo huo wa Chuo Kikuu
Huria na mtu anaweza kusoma alipo na mfumo umekuwa ukiboreshwa siku hadi
siku.
Alisema iliwekwa mifumo ya vyeti na ngazi zake kulingana na vigezo na
hivyo siyo kila cheti kinachotolewa kinaruhusu mtu kwenda ngazi nyingine
na kila mamlaka imepewa jukumu ili kulinda ubora wa elimu unaotolewa
nchini.
Naibu Waziri alisema kutokana na uanzishwaji wa vyuo mbalimbali
kumejitokeza changamoto na watu kutoka katika mfumo rasmi uliopangwa na
kujiwekea mifumo binafsi ambayo imeingiza hata wanafunzi wa kidato cha
nne ambao hawana sifa kuingia vyuo vikuu.
“Jambo hilo limesababisha kuwepo kwa msuguano, haiwezekani mtu afeli
kidato cha nne bila kuwa na cheti kingine chochote anaingizwa katika
kozi hiyo halafu anaingizwa chuo kikuu, sisi hatujarasimisha mfumo huo
wa ‘foundation course’ na hatuna vipimo vyake,” alieleza.
Alisema kwa kawaida mwanafunzi mwenye diploma inayotambulika wamewekewa
usawa wa alama fulani na kidato cha sita hivyo wanakuwa na sifa ya
kuingia vyuo, lakini siyo waliofeli hivyo wanatakiwa kufanya utafiti
zaidi katika kozi hiyo.
“Haiwezekani kila mtu akajianzishia mfumo wake tu, tulifikia eneo ambalo
si zuri kama nchi na sasa tutaimarisha ubora…ukifeli kidato cha nne
unatakiwa kwenda kusoma na kupata cheti kwenye mtaala unaotambulika na
ukaenda diploma na unapofaulu unaweza kwenda chuo kikuu,” aliongeza.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila alisema
suala la ‘Foundation course’ limelenga kumuandaa mtu mwenye sifa ambaye
amekuwa nje ya mfumo kwa muda mrefu ili kuingia chuo kikuu, lakini
walichokuwa wakikifanya wengi ni kuwachukua waliofeli kidato cha nne na
sita na kuwaingiza katika kozi hiyo na hatimaye kuwaingiza chuo kikuu.
Awali, baadhi ya wadau wa elimu nchini waliozungumza na gazeti hili
wakiwemo wanataaluma walisema wanasubiri kupata taarifa rasmi kutoka
wizarani kuhusu madai hayo, lakini wakaeleza manufaa ama athari za
kutumika kwa mfumo huo nchini.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dares Salaam, Dk Benson Bana alisema haamini
iliyonukuliwa ilikuwa kauli rasmi ya serikali, lakini akaongeza, “Upo
utaratibu mbalimbali wa kuingia vyuoni na walio wengi wamepitia mfumo wa
kuanzia cheti na kujiendeleza hadi kufika chuo kikuu na kutunukiwa
digrii wakiwemo maprofesa na madaktari wengi.”
Alisema mfumo huo unasaidia kupata wanafunzi wengi wenye uzoefu na ambao
huwasaidia wenzao katika kufanikisha elimu yao na huo ndio mfumo
unaotakiwa.
Dk Bana alisema jambo linalotakiwa kutazamwa ni uwepo wa vyuo vingi
vikuu ambavyo vimekuwa vikigawa alama za ajabu kwa wanafunzi, lakini
wanapoingia vyuo mtihani ndio utakaowapembua.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch
alisema “Elimu ya kujiendeleza kuanzia ngazi ya cheti na kuendelea
diploma, digrii na hata kufikia uzamivu ni mfumo uliopo dunia nzima.”
Alisema wapo wataalamu mbalimbali nchini na hata maprofesa ambao
hawakusoma katika mfumo huo wakiwamo walimu wake (Ndalichako) waliosoma
kupitia mfumo huo.
Imeandikwa na Hellen Mlacky, Lucy Lyatuu na Regina Kumba-Habarileo.