WAPAMBE WA WASIRA KUKATA RUFAA TENA KUPINGA USHINDI WA ESTHER BULAYA BUNDA MJINI




Baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza kutupilia mbali maombi ya wananchi wanne wa kutaka itengue ushindi wa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini Ester Bulaya (Chadema), walalamikaji hao wamesema watakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kwa kile walichosema kuwa Mahakama hiyo haikutenda haki katika kutoa maamuzi hayo.
Novemba 18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliyokuwa inasikiliza kesi hiyo namba moja ya mwaka huu, katika Mahakama ya Mkoa wa Mara mjini Musoma, chini ya Jaji Noel Chocha, ilitupilia mbali kesi hiyo na kumthibitisha Bulaya kuwa ni Mbunge halali wa jimbo hilo.
Wananchi hao wanne walikuwa wamefungua kesi hiyo wakipinga ushindi wa Bulaya dhidi ya Stephen Wasira kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa waandishi wa habari walimhoji mmoja wa walalamikaji Janes Ezekiel, ambaye alisema kuwa watakaa na wenzake waone namna ya kukata rufaa.
Hata hivyo baadaye mlalamikaji mwingine Ascetic Malagila alimwambia mwandishi wa habari hii kuwa tayari wamekubaliana na wenzake pamoja na mwanasheria wao kuwa watakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu hiyo, kwa kile alichoeleza kuwa wameshindwa kwa sababu ya uonevu na kwamba watatafuta haki yao katika Mahakama ya Rufaa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Wasira alidai kuwa tayari walalamikaji hao pamoja na wakili wao Constantine Mutalemwa, wamekutana na kukubaliana kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kutafuta haki.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa Jaji Chocha, alirejea baadhi ya vifungu vya sheria pamoja na hoja mbalimbali zilizotolewa na waleta maombi (walalamikaji) na wajibu maombi wa kwanza, wa pili na watatu.
Jaji Chocha alisema kuwa kutokana na kupitia vifungu vyote vya sheria pamoja na ushahidi uliotolewa na waleta maombi katika Mahakama hiyo, ni kwamba ushahidi wao haujajitosheleza katika hatua ya kutengua ubunge wa jimbo hilo.
Alisema kuwa iwapo ataamua kufuta matokeo hayo atawasababishia wananchi wa jimbo hilo ambalo ni miongoni mwa jimbo lenye watu masikini sana kukosa haki yao.
Alisema kuwa madhara ya kurudia uchaguzi ni makubwa sana, sanjari na gharama za uendeshaji wa uchaguzi mpya, ambao utaligharimu taifa na wananchi kwa ujumla kwa sababu gharama za uchaguzi ni sehemu ya kodi ya kila mwananchi.
Akirejea mwenendo mzima wa kesi hiyo tangu ilipofunguliwa katika Mahakama hiyo, Jaji huyo alikiri kutokea kwa kasoro kadhaa katika kipindi cha uchaguzi hadi kutangaza matokeo na kusema kuwa ni kawaida ya uchaguzi wowote kuwa na kasoro ndogondogo na kuongeza kuwa hata nchi zilizoendelea kasoro huwa hazikosekani.
Alisema kuwa katika kesi hiyo kasoro nyingi zilizojitokeza zimeonekana mara baada ya matokeo kutangazwa, lakini katika mchakato mzima wa upigaji kura hakuna kasoro zilizobainishwa, ambazo zingeweza kuonekana kwenye fomu yoyote ya malalamiko anayokuwa nayo msimamizi wa uchaguzi, ambazo zingeonesha kuwa uchaguzi haukuwa wa huru na haki. Alibainisha kuwa si kila kasoro inayojitokeza kwenye uchaguzi inaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi.
Hata hivyo alisema kuwa pia msimamizi wa uchaguzi huo Lucy Msoffe alifanya uzembe mkubwa sana wakati alipofika katika hatua ya kuandika idadi ya wapiga kura na kwamba alipaswa kuwa makini kwa kutokuandika takwimu kimakosa.
Akizungumza nje ya Mahakama hiyo wakili wa mjibu maombi Paul Kipeja, alisema maamuzi yaliyotolewa na Mahakama hiyo waliyatarajia tangu mwanzo wa kesi hiyo kwa sababu hakukuwa na hoja zozote za msingi za waleta maombi.
Kuhusu gharama walizotumia katika kesi hiyo wakili Kipeja alisema kuwa watakaa pamoja na wakili Tundu Lissu, ili waweze kurudishiwa gharama zao zote walizotumia kuendeshea kesi hiyo.
Powered by Blogger.