MKATABA WA EPA BALAA...WABUNGE KUAMUA HATIMA YAKE,WADAI HAUNA MASLAHI KWA TAIFA.
Kutokana na hali hiyo wabunge wameitaka Serikali isiingie kwa haraka kwenye mkataba huo kwa kuwa hauna maslahi kwa Taifa.
Mkataba
huo ambao hadi sasa Tanzania haijausaini, unatarajiwa kuwasilishwa
bungeni Alhamisi wiki hii kwa ajili ya kujadiliwa ingawa Kenya na Rwanda
zimekwisha kuusaini.
Akiuchambua
mkataba huo kwenye semina ya wabunge mjini hapa jana, Profesa
Kabudi, alisema mkataba huo haifai kwa kuwa una ahadi nyingi
zisizotekelezwa.
Kwa
mujibu wa mkataba huo, Profesa Kabudi alisema nchi za Ulaya hazitapata
hasara yoyote ila nchi za EAC ndiyo itaathirika kwa sababu
hazitaruhusiwa tena kuongeza ushuru wa bidhaa zinazoingia katika nchi
husika.
“EPA
itasababisha wananchi wa nchi za Afrika Mashariki kukosa ajira kutokana
na ukanda huo kugeuka ukanda huru wa bidhaa za Ulaya.
“Kama
tutausaini kisha tukataka kuingia kwenye ushirikiano wa uchumi na nchi
nyingine zilizo nje ya EPA, mkataba hauturuhusu kwa sababu unalazimisha
nchi za EAC kupeleka kwao bidhaa zenye kuzingatia afya na usalama kwa
kukidhi viwango vya nchi zao.
“Kwa
mujibu wa mkataba huo, kuna uwezekano bidhaa zetu zikakosa soko kwa
kutokidhi vigezo vyao pamoja na kutakiwa kuthibitisha usalama huo
kisayansi ambako kwa bidhaa za nchini ni vigumu kupata uthibitisho huo
kama asali inayotoka Tabora.
“Pia, ibara ya 99 ya mkataba huo inakwenda kuua ajira kwa vijana kwa vile inachagua ni maeneo gani ya kufanyia kazi.
“Uchumi
wa nchi yetu sasa tunaelekeza kwenye mkakati wa viwanda, lakini mkataba
wa EPA una mtego kwa sababu hausemi ni mazao gani ya biashara
yanatakiwa kwao.
“Kwa
hiyo, pamoja na Kenya na Rwanda kuusaini, bado katika jumuiya kama kuna
mwenzenu mmoja hajasaini, hautasainiwa katika jumuiya husika,” alisema Profesa Kabudi.
Mmoja
wa wachambuzi wa mkataba huo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk. John Jingu, alisema Tanzania ikisaini mkataba huo, itapoteza
mapato kwa sababu inategemea ushuru wa forodha ambao asilimia 10 ya
ushuru huo, hutoka kwenye bidhaa zinazoingia kutoka Ulaya.
“EPA
itaiathiri Tanzania katika biashara kwa sababu nchi inazofanya nazo
biashara si za Umoja wa Ulaya kama vile Saudi Arabia, China, India,
Falme za Kiarabu, Afrika Kusini, Uswisi, Marekani, Korea Kusini, Kenya
na Andorra.
Awali,
Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Adolf Mkenda,
alisema Tanzania ikisaini mkataba huo, haitaweza kuongeza kodi na badala
yake itabaki na tozo inazotoza.
Akichangia
mjadala huo, Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), alisema anaunga mkono
uchambuzi wa watoa mada kwa sababu hatua ya kukimbilia kusaini huo ni
kuendelea kuumia.
Mbunge
wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msingwa (Chadema), alisema pamoja na
hoja za uzalendo za wachambuzi hao, bado kuna haja ya kuelezwa pia na
faida zake badala ya kutajwa hasara peke yake.
Mbunge
wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliitaka Kamati ya Bunge
ya Viwanda, Biashara na Mazingira, ihakikishe inakutana na timu ya
wataalamu wakiwamo wafanyabishara kujadili kwa kina mkataba huo.