PAMOJA na Bunge kupitisha Muswada wa
Huduma za Habari wa mwaka 2016 kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka
2016, wabunge kabla ya hatua hiyo waliujadili muswada huo kwa siku
mbili na kutofautiana huku wengi wakionekana kuukubali.
Wabunge
juzi na jana asubuhi wakiujadili muswada huo, baadhi walisema umekuja
kufifisha tasnia hiyo na wengi waliukubali lakini walitaka mambo kadhaa
yaboreshwe ikiwemo kuonesha bayana namna maslahi ya waandishi
yatakavyolindwa na sheria hiyo.
Walisema
kwa nyakati tofauti kuwa waandishi wengi wanakopwa na waajiri wao,
hawalipwi na wakilipwa ni ujira mdogo na wameshindwa kupaza sauti zao
wakiogopa kufukuzwa kazi huku kukiwepo na asilimia 60 ya waandishi ambao
hawajaajiriwa na hakuna wa kuwasemea isipokuwa sheria hiyo.
Muswada
huo uliwasilishwa juzi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye ukiwa na vifungu 62 lakini jana ulipitishwa na
Bunge kuwa sheria ukiwa na vifungu 67 na maboresho katika zaidi ya
vifungu 30 yaliyozingatia maoni ya wabunge.
Katika
majadiliano, wabunge walishauri baadhi ya vifungu virekebishwe zaidi
kikiwemo kifungu cha 56 (cha awali) kinachoipa Polisi mamlaka ya kutwaa
kifaa chochote cha chombo cha habari kama kimekwenda kinyume cha sheria
na kutaka madaraka hayo yarejeshwe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
Mbunge
wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) alisema muswada huo
umekuja kuibana sekta ya habari kwa kuzuia watu wenye ujuzi wa kuandika
kuzuiwa kufanywa hivyo kwa kuwekewa vikwazo vya elimu ya uandishi na
Bodi ya Ithibati.
Zitto
alisema uandishi wa habari ni kazi ya wito akitumia neno ‘passion’ na si
vyema ikawekewa vigezo vya udhibiti kama wanasheria, madaktari na
wahasibu kwa kuwa wako watu katika historia hawakuwa na elimu ya
uandishi lakini ni waandishi wa kuigwa nchini na duniani.
Alimtolea
mfano Mbaraka Islam ambaye alitoa taarifa za kuzama kwa meli ya Mv
Bukoba mwaka 1996 bila kuwa na taaluma ya habari na sasa ni mwandishi wa
mfano. Pia Zitto alimgusia Dk Harrison Mwakyembe (sasa Waziri wa Katiba
na Sheria) ambaye alianza kazi ya uandishi wa habari bila kusomea na
sasa ni mwanasheria mzuri nchini.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu (CCM) aliunga mkono
muswada hasa maeneo yanayozungumzia mwandishi kukatiwa bima na kuwepo
kwa Mfuko wa Habari utakaohusika kufadhili waandishi kusoma kozi fupi na
ndefu.
Adadi, alisema
waandishi wa habari wanafanywa kama vibarua na baadhi ya wamiliki na
wanakosa haki zao. Alisema nusu ya waandishi hawalipwi wala hawana barua
za ajira na wanaogopa kutoa taarifa, wanaogopa kufukuzwa kazi.
Pamoja
na hilo, Adadi aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai (DCI), kabla ya kuwa Balozi wa Tanzania, Zimbabwe, alisema kuna
watu wanang’ang’ana kuwa muswada huo ni mbaya ili kuzuia waandishi wa
habari wasipate haki zao.
Adadi
alitaka muswada ulinde maslahi ya waandishi wa habari wazawa na wageni
na kuunga mkono uwekezaji wa asilimia 49 wa vyombo vya habari kwa raia
wa kigeni nchini dhidi ya asilimia 51 ya wazawa na kutaka wabunge wajue
hakuna sheria isiyompa waziri mamlaka ya kusimamia mambo fulani kwa
mujibu wa kanuni.
“Nashauri
madaraka ya Mkurugenzi wa Mashitaka yarejeshwe badala ya kuachia Polisi
kuchukua hatua ya mambo yote yanayohusika na uchochezi,” alisisitiza
Adadi.
Naye Mbunge wa
Mafinga, Cosato Chumi (CCM) ambaye kitaaluma ni mwandishi, alishauri
muswada uzungumzie asilimia 60 ya waandishi (correspondent)
wanaofanyakazi kwa maslahi duni na kutaka utetee maslahi ya waandishi
kulipwa na kutonyanyaswa na wamiliki wa vyombo vya habari.
Mbunge
wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) yeye alishauri kipengele
kinachowanyima waandishi uhuru wa kupata habari kutoka vyanzo mbalimbali
kifutwe kwa kuwa kinaminya uhuru wa habari Kikatiba.
“Kipengele
namba 20 kifungu kidogo cha tatu kifutwe kabisa ni kibaya. Naipongeza
serikali kwa kufuta kifungu namba 50 (4) naomba na kipengele cha nane
nacho kiondolewe kabisa,” alisema Bashe.
Akichangia,
Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema) alisema atapeleka marekebisho
katika muswada huo kutokana na kutokubaliana na mambo kadhaa na kutaja
miongoni mwake kupinga wanahabari kuwa na mavazi maalumu na kuzuiwa
wageni kumiliki asilimia 100 ya hisa kwenye chombo cha habari.
Mbunge
wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM) alisema tasnia ya habari
haijawahi kupata heshima inayostahili kwa wanahabari na wamiliki wa
chombo cha habari lakini muswada huo sasa utawapa heshima hiyo kutokana
na mageuzi yaliyofanywa ili wanahabari wawe na hadhi kama ilivyo kwa
wahandisi na madaktari.
“Nahisi wabunge wa upinzani mnataka uandishi wa habari uwe kama shule ya chekechea na usifike chuo kikuu...,” alisema.
Naye
Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Mmasi (CCM) alimtaka Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape kuweka kwenye kanuni mambo yanayofaa
kuandikwa na yasiyofaa kuandikwa kwenye vyombo binafsi vya habari ili
kuepuka mambo yasiyofaa kwenye tamaduni za kitanzania.
Kwa
upande wa Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya Salum (CCM) alisema Mfuko wa
Mafunzo wa kuendeleza wanahabari utengewe fedha haraka na pia wanahabari
wa vyombo binafsi wapate nafasi ya kusaidiwa na mfuko huo kwenye
mafunzo.
Sheria hiyo
inasubiri saini ya Rais John Magufuli ianze kutumika baada ya kutungwa
kwa kanuni na Bunge kuridhia. Tayari Rais akizungumza na waandishi wa
habari juzi, alisema atasaini sheria hiyo siku hiyo hiyo
itakapowasilishwa mezani kwake.
Imeandikwa na Gloria Tesha-HabarileoDodoma |