Makala: Bodi ya Ithibati ya Wanahabari haitazuia uhuru wa habari.
![]() |
Wanadamu wameumbwa
kwa hulka na silika ya kuwa na uwezo wa kuwasiliana miongoni mwao, jamii
wanamoishi, taifa na hata ulimwenguni ili waweze kutimiza nia na azma yao ya kuwasiliana.
Ili mawasiliano hayo yakamilike ni lazima yabebe ujumbe unaokusudiwa kufikishwa katika jamii.
Ujumbe huo ili
uweze kumfikia mlengwa, ni lazima iwepo njia ya kuufikisha ujumbe huo
kwa mlengwa ambao huwasilishwa kwa maandishi (magazeti), sauti (redio)
na picha (TV) pamoja na mitandao ya kijamii kupitia huduma ya inteneti.
Vyombo hivyo
vya habari vinahusisha wataalamu ambao kazi yao ni kuhakikisha jamii
inapata ujumbe kwa wakati ili kuweza kujenga, kuboresha na kuimarisha
maisha yao kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Vyombo vya
habari hakika vimekuwa ndio macho na masikio ya wananchi ili kufikisha
ujumbe unaohusu mambo mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya nchi.
Uanzishwaji wa
Bodi ya Ithibati ya Wanahabari kama ilivyoainishwa katika Muswada wa
Huduma za Habari wa mwaka 2016 hautaminya uhuru wa kutafuta na kusambaza
habari.
Msingi wa haki
ya kutafuta taarifa na kusambaza habari unatokana ibara ya 18 ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo watu wasiwe na hofu ya kuwa
Bodi hiyo itawaminya watu kutoa mawazo yao.
Bodi ya
Ithibati ya Wanahabari haiwezi kuwa kizuizi cha watu kutafuta na
kusambaza habari kwani haki hiyo ipo kikatiba kupitia ibara ya 18 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Sioni sababu
yoyote ya kupinga uanzishwaji wake kwa kuwa malengo yake ni kuhakikisha
inasimamia kanuni za maadili ya wanahabari hapa nchini na kuijengea
heshima tasnia.
Pamoja na
kuanzishwa kwa Bodi hiyo hakuna maana kwamba uanzishwaji wake utachukua
majukumu ya taasisi zingine za habari zilizopo na kuongeza kuwa
waandishi wa habari duniani kote wanafanya kazi kwa kufuata miiko ya
maadili ya uandishi wa habari.
Suala kubwa kwa
mwanahabari ni kuzingatia maadili na weledi wa taaluma yake ili
kutekeleza majukumu yake pasipo kusababisha usumbufu kwa mtu au kikundi
kingine.
Muswada huu
umeandaliwa kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika tasnia
ya habari nchini ambazo ni pamoja na upungufu wa sheria zinazosimamia
tasnia hii na mabadiliko ya teknolojia ya habari.
Changamoto ya
kutokuwepo kwa udhibiti mzuri na usimamizi madhubuti ya viwango kwenye
taaluma ya habari na utangazaji kumechangia madhila kwa jamii ikiwemo
kuandikwa habari za upotoshaji, zinazokiuka maadili na zinazoweza
kusababisha chuki, machafuko na uvunjifu wa amani.
Kutokana na
mwingiliano wa teknolojia, mwaka 2003 serikali iliona umuhimu wa
kuunganisha vyombo viwili; Tume ya Mawasiliano na Tume ya Utangazaji ili
kuleta ufanisi wa usimamizi wa sekta na utoaji wa huduma bora kwa
walaji.
Kwa ujumla
sekta hii changamoto kubwa ni taaluma ya habari kutotambulika kama
taaluma kamili inayopaswa kuheshimiwa, kukosekana vyombo madhubuti na
huru vya usimamizi na badala yake mambo mengi kuwa chini ya serikali
moja kwa moja.
Sheria hii
inaleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa sekta ya habari hapa nchini
ni sheria ambayo inakwenda kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi
yetu, kuifanya rasmi sekta ya habari kuwa sekta rasmi.
Wengi wamekuwa
waathirika wa uandishi usiozingatia maadili na weledi wa taaluma ya
habari na utangazaji kwa kukashifiwa au kuzushiwa taarifa zisizokuwa na
ukweli wowote.
Mapendekezo
yaliyomo katika sheria ya habari kwa kiasi kikubwa yamelenga kutatua
changamoto ya kuwa na wanahabari waliosomea kazi yao na ambao
wamewekeana maadili ya kufuata.
Ni sheria itakayoleta mifumo ya kisasa ya usimamizi na ni mifumo ambayo inaweza kugusa au kubadili namna tutakavyotenda na tunavyofikiria sasa.
Ni sheria itakayoleta mifumo ya kisasa ya usimamizi na ni mifumo ambayo inaweza kugusa au kubadili namna tutakavyotenda na tunavyofikiria sasa.
Niwaombe wanatasnia wenzangu tuwe tayari kwa mabadiliko ili taaluma yetu iheshimiwe na sisi wenyewe tuheshimike zaidi.
Na Loyola, Habari maelezo
