Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB),
imetangaza awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na
vyuo vya elimu ya juu nchini watakaopewa mkopo kugharimia masomo yao.
Idadi ya wanafunzi ambao tayari wamepitishwa kupata mkopo ni
7,904, hata hiyo imeelezwa kiwango hicho kitaendelea kubadilika kwa kuwa
mchakato unaendelea.
Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia, Stella Manyanya ilibainisha kuwa bodi imekamilisha uchambuzi wa
majina ya waombaji ambao wana sifa zinazotakiwa na majina ya wanufaika wapya
ambayo yameanza kutangazwa kupitia tovuti ya bodi hiyo.
“Kwa kuzingatia mpango mkakati,
pia mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka 2016/17, Serikali imetoa vigezo
vitakavyozingatiwa katika utoaji mikopo,” alisema Manyanya.
Alitaja vigezo vilivyotumika kuwa ni pamoja na vipaumbele
vya kitaifa vinayoendana na mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2025 na mafunzo ambayo yatazalisha wataalamu wanaokidhi
mahitaji ya kitaifa katika fani za kipaumbele.
Manyanya alizitaja fani zilizopewa vipaumbele kuwa ni
sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda,
kilimo, mifugo, mafuta na gesi asilia, sayansi asilia na mabadiliko ya
tabianchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Katika taarifa yake, Manyanya alisema pia mchakato wa
kuwapata wenye sifa za kukopa uliangalia uhitaji wa waombaji, hususan wenye
mahitaji maalumu kama walemavu na yatima, ufaulu wa waombaji katika maeneo ya
vipaumbele na umahiri.
“Kuanzia mwaka huu wa masomo, wanufaika wote wa mikopo (wapya na
wanaoendelea na masomo) watakopeshwa kulingana na uwezo wao katika vipengele
vyote vya mikopo,” alisema.
Akizungumzia mchakato huo, mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo,
Abdul Badru alisema unaendelea kufanywa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na
timu ya bodi imejigawa katika vikundi ili kuhakikisha mipango inakwenda jinsi
inavyotakiwa.
“Timu ipo kazini na inafanya kazi
yake kwa umakini. Kwa sasa majina ya waliochaguliwa kutokana na vigezo
yamewekwa, lakini ni wahusika wenyewe au walezi na wazazi ndiyo wanaweza
kuyaona kupitia namba zao za usajili wa kidato cha nne. Lakini siku chache
zijazo tunaweza kuwataja wakaonekana kwa kila anayehitaji kuyaona,” alisema Badru.
|