WANANCHI wanaoishi mpakani mwa Msumbiji
na Tanzania wameiomba serikali kukomesha biashara ya ngono kwa watoto
chini ya miaka 18 katika mji wa machimbo wa Dar Pori.
Walitoa
ombi hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mpaka wa
Msumbiji na Tanzania katika kata ya Unyere, Tarafa ya Mpepo
uliohudhuriwa na viongozi wa Msumbiji na Tanzania.
Katika
mkutano huo Mkuu wa Mkoa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge alikuwa mgeni
rasmi. Wazazi hao walizitaka serikali za pande zote mbili kudhibiti
mpaka na kuwakemea watu wanaowaingiza watoto walio chini ya miaka 18
katika biashara ya ngono.
Mzazi
mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Mohamed alisema wao wakiwa
kama wazazi wanaona huruma kwa watoto walio chini ya miaka 18 wakifanya
kazi za ngono ili waweze kujikimu kimaisha.
“Watoto
hawa wanachukuliwa wakidaiwa wanakwenda kufanya kazi za majumbani,
kumbe wanaenda kufanya kazi za baa kwa malipo ya mlo mmoja , mlo
mwingine wajitafutie na mtu akifika dau anamlipa anayewahifadhi,”
alisema mzazi huyo na kuongeza kwamba mwenye baa analipwa kati ya
shilingi 20,000 na Sh 50,000 kutegemea urembo wa binti mhusika.
Dar-Pori,
mji uliochipuka kutokana na kuwapo kwa machimbo ya dhahabu unasifika
kwa ngono toto kama sehemu ya burudani baada ya kazi nzito.
Aidha
biashara hiyo inafanyika upande wa pili wa mpaka ambapo wasichana hao
wadogo huvuka kwa maelezo kwamba wanakwenda kutembelea ndugu zao na
kuishia katika madanguro yanayohifadhi watu kuanzia 10 hadi 20.
Kwa
sasa dhahabu inapatikana kwa wingi upande wa pili na kufanya kuwapo na
machimbo manne yanayotumika kutafuta dhahabu huku wachimbaji wake wakiwa
ama Tura au Dar–Pori.
Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge akijibu hoja hizo alisema
biashara ya kusafirisha binadamu ni kinyume cha sheria na kwamba mtu
atakayekamatwa atafikishwa mahakamani.
Aidha
alipiga marufuku biashara hiyo ya kusafirisha watoto ambao
wanatumbukizwa katika kumbi zao za starehe ili kuwafanya kivutio na
chambo ili kufanikisha biashara zao. Aliwataka viongozi wa vijiji,
watendaji pamoja na wananchi wa kawaida kuingia katika vita ya kupambana
na biashara hiyo haramu ya kusafirisha watoto kwa madhumuni ya
kuwatumbukiza katika biashara ya ngono.
Viongozi
wa Msumbiji wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wachimbaji Msumbiji, Alexanda
Ndekiso walimuahidi Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kuwa watakomesha biashara
hiyo na kuwarudisha watoto walio chini ya miaka 18 ambao wanatumika
kwenye biashara hiyo.
Walisema
watafanya kila njia kuhakikisha watoto wanaohitajika kuwa shuleni
wanarudishwa Tanzania ili waweze kushiriki masomo, jambo lililoungwa
mkono na mkuu wa askari wa mpakani Komezi Amanzi. | |