Wahadhiri UDOM wafunguka sababu ya Mgomo chuoni hapo
Jumuiya ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu
cha Dodoma (UDOMASA) imesema kilichotokea si walimu kugoma kufundisha programu
ya Stashahada Maalumu ya Elimu, Sayansi, Hisabati na Tehama, bali tatizo ni
kutoelewana na Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji
wa programu hiyo chuoni hapo.
Aidha, imelaani kitendo cha
wanafunzi 7,802 wa Programu Maalumu ya Ualimu wa Msingi na Sekondari,
waliorudishwa nyumbani bila kupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa kuzingatia
umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi, hali inayofanya wazagae mitaani huku
wakiwa hawana pa kwenda.
Hayo yako kwenye tamko lililotolewa
jana na Katibu wa jumuiya hiyo, Lameck Thomas, ambalo lilieleza kuwa lawama zimekuwa
zikitupwa kwa walimu kutokana na taarifa hizo kutolewa na upande mmoja, ambao
ni Menejimenti ya chuo kwenda serikalini bila kuwepo na taarifa yoyote kutoka
kwa walimu kupitia jumuiya yao.
Thomas alisema si kweli kama walimu
waligoma kufundisha lakini tatizo kubwa ni kutoelewana kati ya walimu na
Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo
chuoni hapo.
“Hatuzungumzii fedha zaidi
tunazungumzia suala la kuboresha elimu ili taifa lipate walimu wa baadaye
katika kufundisha Sayansi, Hisabati na Tehama, vifaa vya kufundishia navyo ni
changamoto kubwa,” alisema.
Katibu huyo alisema kama Jumuiya ya
Wanataaluma wanapata hisia kwamba Wizara ya Elimu, imeamua kwa makusudi
kushirikiana na uongozi wa chuo kupotosha uhalisia wa jambo hilo kwani hakuna
hata wakati moja ambao wamefanya mawasiliano na walimu wenyewe kupata ukweli
kutoka upande wao.
“Alichosema waziri bungeni juzi ni
taarifa ya upande mmoja ambayo haitatupeleka kwenye utatuzi wa kudumu wa suala
hili kutokana na ukweli kwamba walimu nao wana mengi ya kuzungumza,” alisema katibu huyo.
Alisema serikali imejenga desturi ya
kuonana na menejimenti za vyuo pindi yanapotokea matatizo bila kupata taarifa
kutoka vyanzo vingine hali ambayo imekuwa inasababisha vyanzo sahihi vya matatizo
kutojulikana kwa uwazi.
Alisema changamoto za ufundishaji
kutokana na uhaba na walimu kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo. Akitoa
mfano alisema kwa sasa Chuo cha Sayansi Asilia na Hesabu, kina upungufu wa
walimu 128 waliokuwa wanahitajika kufundisha programu hiyo kwa ufanisi; na kwa
muhula uliopita walimu 72 tu ndio walibeba mzigo wa upungufu huo na muhula huu
hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya zaidi.
“Wingi wa wanafunzi na uhaba huu wa
walimu ulisababisha upangaji wa ratiba na kufundisha kutokana na ukweli kwamba
kozi ziligawanywa katika mikondo mingi ambayo walimu walilazimishwa kuifundisha
huku wakiwa na majukumu ya kufundisha kozi za shahada na majukumu mengine,” alifafanua.
Alisema chuo kimekuwa na desturi ya
kupokea wanafunzi wengi bila kuzingatia idadi ya walimu waliopo na miundombinu
ya kufundishia na kujifunzia na hiyo si mara ya kwanza kwa chuo kufanya hivyo,
kwani mwaka 2008 walileta wanafunzi wengi ambao matokeo yake walimu kufundisha
masomo mengi kuliko uwezo wao wa kazi.
Alisema taarifa iliyotolewa na Ofisi
ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma ilipotoshwa, kwani haijaeleza ukweli wa
madai uliowasilishwa na chuo husika.
Alisema katika Chuo cha Sayansi
Asilia na Hesabu taarifa inasema yaliyowasilishwa ni madai ya Sh milioni 367.8
na kupungua mpaka Sh milioni 90 wakati uhalisia ni kwamba madai hayo hata
yangebanwa namna gani yasingepungua mpaka chini ya Sh milioni 223.7.
Alisema mfano mwingine ni Chuo cha
Elimu Masafa na Sayansi za Kompyuta ambao taarifa inasema waliwasilisha madai
yanayozidi Sh milioni 100 wakati taarifa ya chuo inasema ni madai ya Sh milioni
53.7 tu.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Edson
Baradyana alisikitishwa na yaliyotokea na kuitaka serikali kufanya jitihada za
makusudi ili kumaliza mgogoro huo na hilo litawezekana kama walimu, wanafunzi
na Menejimenti kukaa pamoja.
Baradyana alisema wanafunzi
hawakutendewa haki kwani ilitolewa notisi ya ghafla ya kuondoka chuoni huku
wengine wakiwa hawana nauli na hawakujua pa kwenda hali inayofanya waendelee
kuzurura mitaani.
Alisema wanaamini kama Menejimenti
ya chuo ingeonesha ushirikiano wa karibu kwa walimu wanaofundisha programu hiyo
na kushirikiana, hayo yasingetokea au yasingekuwa makubwa kiasi hicho.
“Lazima kuangaliwa na kutatuliwa kwa
changamoto nyingine zilizoibuliwa na wanataaluma na wanafunzi katika uendeshaji
wa programu hiyo badala ya kujikita kwenye suala la malipo tu, serikali iwe na
utaratibu wa kuwasiliana na walimu na wanafunzi mara kunapotokea matatizo
vyuoni ili kupata taarifa toshelezi kutoka pande zote,” alisema Mwenyekiti wa Udomasa.
Aidha, wakati wa kurejeshwa nyumbani
kwa wanafunzi hao wa Udom kukibebwa kisiasa na vyama vya upinzani, taarifa ya
serikali imeeleza kuwa wahadhiri waliogoma, walitaka kulipwa posho ya zaidi ya
Sh milioni 900.
Akitoa taarifa ya pili bungeni juzi
usiku, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako alisema wanafunzi hao si sehemu ya kazi zilizoko katika
mikataba ya ajira ya wahadhiri hao, ila ni sehemu ya kazi ya ziada.
Kwa kuwa kazi hiyo ni ya ziada, Profesa
Ndalichako alisema walikubaliana walipwe posho ya kazi ya nyongeza ambayo
uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ulikuwa tayari kutoa zaidi ya Sh milioni 200.
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako,
wahadhiri hao walisisitiza kuwa wanataka posho hiyo iwe zaidi ya Sh milioni
900, jambo lililokataliwa na Mkaguzi wa Ndani wa Mahesabu wa Udom aliyesema
kuwa kiwango hicho ni kikubwa kuliko uhalisia wa kazi yenyewe.
Kutokana na kutokubaliana kati ya
wahadhiri hao na uongozi wa Udom, wahadhiri hao ndio wakaitisha mgomo wa
kufundisha wanafunzi hao huku wakiendelea na kazi za kufundisha walio katika
programu za shahada ya kwanza na kuendelea.
Profesa Ndalichako alisema kwa
uamuzi huo wa wahadhiri, serikali isingeweza kuwachukulia hatua kwa kuwa
wamegomea kazi ya ziada na si kazi waliyoajiriwa na kuingia mkataba na chuo.
Kwa hali hiyo, Profesa Ndalichako
alisema serikali ililazimika kuingilia kati ambapo Mei 10, mwaka huu Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya
alikwenda chuoni hapo kutafuta suluhu.
Mbali na Naibu Waziri, alisema hata
makatibu wakuu wa wizara hiyo nao walikwenda kuzungumza na wahadhiri hao bila
mafanikio, huku wanafunzi hao wakikaa chuoni bila kuingia darasani kwa wiki ya
tatu.
Profesa Ndalichako alisema mbali na
madai ya wahadhiri hao, pia wakati wa kutafuta suluhu ya jambo hilo, walitazama
suala la tija kwa wanafunzi hao wa diploma maalumu ambao ni zaidi ya 7,800 na
pia kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza ambao pia wanapaswa kufundishwa na
wahadhiri hao.
Kutokana na kukosa masomo kwa wiki
tatu mfululizo na kuwepo kwa uwezekano wa kukosekana tija katika ufundishaji,
Profesa Ndalichako alisema ndio uamuzi wa kuwarudisha nyumbani wanafunzi hao
ukafanyika ili serikali iangalie upya utaratibu wenye tija zaidi wa kuwaendeleza
wanafunzi hao.
Aidha, Profesa Ndalichako alisema
wakati wanafunzi hao wakitakiwa kurudi nyumbani, walizingatia hali yao ya
kipato, kwa kuwa tayari walikuwa wameshapewa fedha za kujikimu za siku 60 tangu
Aprili 21, mwaka huu.
Profesa Ndalichako aliwataka
wanafunzi hao kuvuta subira wakati serikali inatafuta namna bora ya kuwapatia
elimu hiyo kwa kuzingatia tija kwao.