SERIKALI imesitisha ajira zote, kama njia ya kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Kutokana na uamuzi huo hivi sasa hakuna nyongeza ya mishahara kwa
watumishi wa Serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali wa
likizo ya bila malipo.
Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, jana alisema kuwa Serikali
imesitisha kwa muda utoaji wa ajira, ili kupitia upya muundo wa
Serikali na taasisi zake.
Alisema utekelezaji wa mkakati huo utakwenda sambamba na kusitisha kwa
muda utoaji wa vibali vya ajira zote mbadala pamoja na uidhinishaji wa
ajira hizo zilizopo Sekreterieti ya Ajira katika utumishi wa umma na
kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi.
“Ni kweli tumesitisha kwa muda ili kupitia mfumo wa Serikali na hata
kuangalia ulipaji wa mishahara kama upo katika malipo stahiki.
“…na hili litakwenda sambamba na hata kusitishwa malipo ya mishahara
yanayotokana na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi. Tukimaliza zoezi
hili ndipo tunaweza kuanza kutoa ajira za Serikali,” alisema Dk.
Ndumbaro.
Alisema muundo mpya wa utumishi wa Serikali unakwenda sambamba na
uhakiki wa malipo ya mishahara, hivyo ni lazima ujue ni nani unayemlipa
kuliko ilivyo sasa.
Kwa mujibu wa maelekezo hayo uhamisho na uidhinishaji katika mfumo wa
watumishi ambao wamehamishwa kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwajiri
mwingine ambao atalipwa mshahara mkubwa kuliko ule wa sasa pia
utaangaliwa kwa lengo la kupata taarifa sahihi za mtumishi husika.
“Baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki watumishi pamoja na tathmini
ya muundo wa Serikali na taasisi zake, wote wataarifiwa ni lini
utekelezaji utaendelea,” alisema.
Taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini, zinaarifu kuwa maelekezo hayo
yalitolewa Juni 13, mwaka huu na kusambazwa katika maeneo mbalimbali
ikiwemo kwa makatibu wakuu wote, makatibu tawala wa mikoa, kwa wakuu wa
idara za Serikali zinazojitegemea.
Waliotakiwa kutekeleza maelekeo hayo ya Serikali ni wakurugenzi wote wa
majiji, manispaa na miji, wakurugenzi watendaji wa halmashauri za
wilaya, watendaji wa taasisi za umma na watendaji wa wakala za Serikali
kwa upande wa Tanzania Bara. Kamatakamata Wiki iliyopita vyombo vya dola vilianza kuwatia mbaroni watumishi hewa kwa kuwafuata na pingu majumbani.
Hatua hiyo imetajwa kuwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano chini
ya Rais Dk. John Magufuli, kuanza kupambana na watendaji ambao wamekuwa
wakiisababishia hasara Serikali ya kulipa mamilioni ya shilingi kwa
watumishi hewa.
Kutokana na uamuzi huo ambapo mtumishi mmoja wa moja za Mkoa wa
Kigoma, alifuatwa na askari wa polisi na kutiwa mbaroni nyumbani kwao
Ubungo Kibangu jijini Dar e Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea mchana wa juzi na kuibua hisia
miongoni mwa majirani ambao waalisema kuwa, askari hao walifika nyumbani
kwao na mtumishi huyo na kumfunga pingu mikono na miguuni na kuondoka
naye.
Kutokana na hekaheka hiyo ya watumishi hewa, taarifa kutoka wilayani
Nyasa mkoani Ruvuma, zilidai kuwa walimu watano wastaafu nao walikamatwa
na polisi kwa madai ya kupokea mishara hewa.Mbali na walimu hao pia
alikuwepo muuguzi mmoja.
Hivi karibuni akizungumza Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki,
alisema Serikali imewaondoa jumla ya watumishi 12,246 kwenye mfumo wa
malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali, ikiwemo umri wa kustaafu kwa
lazima, kufukuzwa kazi, vifo na kumalizika kwa mikataba. Waziri Kairuki alisema kuondolewa kwa watumishi hao kumeokoa Sh bilioni 25 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao.
Alisema kuwa fedha hizo zingepotea endapo watumishi wasingeondolewa
kwenye mfumo, ikilinganishwa na watumishi 10, 295 walioondolewa kwenye
mfumo kuanzia Machi 15 hadi Aprili 30 mwaka huu. Alisema pia kuwa watumishi hewa 1,951 wameongezeka ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 1.8.
Alifafanua kuwa ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu
wa taasisi za umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwasilisha taarifa
ya watumishi hewa ifikapo Juni 10, mwaka huu. Chanzo: Mtanzania
|