Waziri Jafo Atoa Siku Tano Kwa Halmashauri 10 Kujieleza Kuhusu Matumizi Ya Fedha Za Miradi Ya Afya
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Seleman Jafo ametoa siku tano kwa
wakurugenzi na waganga wakuu wa halmashauri 10 nchini kutoa maelezo ya
kina kwa nini halmashari hizo hazijafika asilimia kumi ya matumizi ya
fedha za miradi ya afya.
Jafo
ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao kazi juu ya utekelezaji wa
miradi ya afya inayotekelezwa chini ya Mamlaka za Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa kilichowajumuisha Makatibu Tawala kutoka mikoa yote
nchini.
Amesema
halmashauri hizo zimeshindwa kutumia fedha zilizotolewa kwa ajili ya
miradi ya afya kama inavyotakiwa ambapo matumizi yake yanaonekana kuwa
chini ya kiwango, huku akizitaja halmashauri hizo kuwa ni halmashauri ya
wilaya ya Karatu, Mpimbwe, Mbulu Dc, Songwe, Simanjiro, Mkinga,
Mkuranga, Namtumbo, Nzega TC pamoja na Kilindi.
“Halmasharu
hizi zina kila dalili ya kupata hati chafu, naagiza hadi kufika siku ya
Jumatano niwe nimepata majibu ya kuridhisha ni kwanini hawajatumia
fedha walizopewa kama maelezo yanavyotaka, tukiacha kufanya kazi kwa
mazoea tutapata matokeo mazuri, lakini kwa hali hii tusitegemee matokeo
mazuri kwa baadhi ya maeneo” Alisema Jafo
Kuwa
upande mwingine Waziri Jafo aliwaagiza Makatibu Tawala hao kuwaelekeza
wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwekeana malengo na watumishi wao kwa
kuwafanya tathmini ya uwajibikaji kila mwaka ili kuongeza ufanisi na
uwajibikaji kazini kwani bado wapo baadhi ya watumishi wanafanya kazi
kwa mazoea.
Amesema
kuwa iwapo mtumishi wataonekana amefanya kazi chini ya kiwango cha
alama 50 kama ni mkuu wa idara atawajibishwa kwa kushushwa cheo, na yule
ambaye ataonekana kufanya vizuri zaidi alishauri anastahili kupewa
zawadi ya mfanyakazi bora wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi
Duniani-Mei Mosi.
Aidha
Waziri Jafo amesema kwa sasa kipaumbele cha utoaji wa fedha kwa ajili
ya miradi ya maendeleo zitatolewa kwa kuzingatia kipimo cha matokeo
mazuri kwa halmashauri husika, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia
kuongeza uwajibikaji.
Wakati
huo huo Waziri huyo aliagiza halmashauri zote nchini kuweka mfumo wa
matumizi ya mfuko wa afya ya jamii wa CHF iliyoboreshwa sambamba ya
kuhimiza matumizi ya ukusanyaji wa mapato wa njia ya kimtandao ili
kuepuka upotevu wa fedha za serikali.
Akizungumzia
mafanikio ya mfuko huo Mratibu wa mfuko wa afya ya jamii TAMISEMI,
Nkinda Shekalaghe amesema kuwa hadi sasa mfuko huo haujafikia lengo
lililowekwa na serikali la kuunganisha wananchi kwa asilimia 30 hadi
kufikia mwaka 2015, kwani kwa mwaka 2016/2017 wamefikia asilimia 24.
Alitaja
baadhi ya changamoto zinazoukabili mfuko huo kuwa ni pamoja na utayari
wa wananchi kujiunga na mfuko, huduma duni za afya, kutokuwepo kwa mfumo
rasmi wa utoaji wa taarifa pamoja na kiwango kidogo cha uchangiaji
ambapo amesema tayai wameshachukua hatua mbalimba katika kukabiliana na
changamoto hizo.