OSMAN WA EVERTON BADO ANAWAKUMBUKA DROGBA, ETO’O, BOSI WAKE AIELEZEA TANZANIA
Na Saleh Ally
TANZANIA imepata ugeni wa wadau wa soka ambao inawezekana kila kiongozi au mchezaji angependa kujifunza kupitia kwao.
Hao
ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Everton ya England, Robert Elstone
pamoja na mchezaji gwiji wa klabu hiyo, Leon Osman, mmoja wa viungo
waliocheza mechi nyingi zaidi wakiwa na Everton.
Osman
amecheza mechi 400 akiwa na kikosi cha Everton na yeye pamoja na bosi
wake, walikuwa Tanzania kwa siku mbili katika mkutano wao na uongozi wa
SportPesa Tanzania.
SportPesa sasa ndiyo wadhamini
wakuu wa Everton ambayo msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya saba
nyuma ya Manchester United na Elstone anaamini wanaweza kujipanga zaidi.
Everton
itakuwa nchini Julai 13, kucheza na bingwa wa SportPesa Super Cup
ambaye atapatikana baada ya michuano itakayoshirikisha timu za Kenya na
Tanzania.
Mahojiano
maalum kupitia SALEHJEMBE pamoja na Elstone, baada ya hapo alifuatia
Osman ambaye alizungumzia mambo kadhaa ikiwemo kuhusiana na wachezaji
Waafrika anaowakubali zaidi.
Swali: Baada ya kutua Tanzania umeona mambo kadhaa, nini umejifunza?
Elstone: Kwanza ni tabasamu, watu wenye mapenzi na furaha, lakini wameonyesha wengi wanapenda soka hasa.
Swali:
Kuna mjadala kuhusu Everton kusafiri hadi Afrika na hasa Tanzania kwa
ajili ya maandalizi ya msimu mpya, watu wanaona kama mmekosea?
Elstone:
Sisi tunachukulia kama ni utambulisho wa Everton kwa Afrika Mashariki
na Tanzania, kupata mashabiki wapya na kuwaeleza wadau tunafanya nini.
Pia tuna nafasi ya kujifunza na ndiyo maana wanaweza kutoa maoni lakini
sisi tunaweza kujifunza zaidi.
Swali: Kitakuwa ni kikosi kizima cha kwanza?
Elstone: Kocha Koeman ataleta kikosi kizima na tunaamini itakuwa ni furaha kujumuika pamoja.
Swali: Mtacheza na bingwa wa SpotPesa Super, mnaona mambo yatakuwa laini?
Elstone:
Hatuamini hivyo, tunaona ni nafasi nzuri kwetu kupambana. Tunaamini
kutakuwa na ushindani pia ni jambo zuri kwa SportPesa walioamua kuandaa
mashindano kumpata bingwa.
Swali: Baada ya mechi, mtamalizia kambi yenu ya maandalizi hapa Tanzania, au mtaondoka?
Elstone:
Hapana tutaondoka kurudi nyumbani, tunakwenda kwenye upande wa pili wa
maandalizi. Kumbuka tunajiandaa na sehemu ya mtoano kuwania kucheza
Europa League. Pia tuna mchezo dhidi ya Sevilla. Kila siku kwetu ni
muhimu na lazima tuitumie vizuri.
Swali: Everton inaonekana nafasi yenu ni ya sita, saba. Vipi mnafanya nini siku moja tuone mkiwa mabingwa au angalau namba mbili?
Elstone:
Tunapambana sana kufanya vizuri, kila mtu anapambana na lengo ni
kubadili mambo. Angalia kuna mwekezaji mpya, anaonekana amepania kufanya
vema. Sasa angalia ishu ya uwanja mpya imeanza lakini bado lengo ni
kuifanya Everton izidi kuwa bora na bora zaidi.
Tunaendeleza vijana, tuna akademi bora kabisa ambayo tunaamini baadaye ni ukombozi.
Swali: Wewe ni mhasibu kitaaluma, umeona chochote kama biashara mara baada ya kufika hapa?
Elstone:
Ninaamini kwa kuungana na SportPesa tutafanya kazi ya kuitambulisha
Everton kwa watu wa Tanzania na Afrika Mashariki. Tutazidi kuongeza
nguvu kundi la wanachama kupitia hapa. Watu wataijua zaidi klabu yetu,
nasi tutajifunza zaidi kuhusiana na ukanda huu na hii ni njia nzuri ya
biashara.
Baada
ya Elstone, ilikuwa zamu ya Osman, gwiji huyu wa Everton aliyewahi
kucheza timu ya taifa ya England na mmoja wa wachezaji wenye heshima
kubwa katika klabu hiyo.
Hata
hivyo, wenyeji wao waliendelea kushikilia msimamo wa kutowauliza
maswali yoyote ya usajili kwa kuwa wasingejibu kama lile la Wayne Rooney
kurejea, Lukaku kuondoka au wamepanga kumuacha na kumsajili nani
wakitaka zaidi iwe kuhusiana na ziara yao, haikuwa na ujanja.
Osman
sasa ana miaka 36 na alistaafu kuichezea Everton msimu uliopita akiwa
mmoja wa manahodha. Alifunga mabao 43 akiwa na Everton.
Swali: Mechi 400 katika Premier League si jambo dogo, uliwezaje?
Osman:
Siwezi kusema ninajua sana, lakini ni hamu ya mafanikio. Nilitaka
kufanya zaidi na zaidi. Nilitaka mechi moja, baadaye nikataka tano na
mwisho nikataka kufikisha 400. Kwa kifupi nilitaka mafanikio zaidi.
Swali: Unaweza kutuambia wachezaji bora kutoka Afrika uliocheza kwenye timu yako au Ligi Kuu England?
Osman:
Wako wengi lakini Samuel Eto’o na Didier Drogba. Nilicheza na Eto’o,
alinipa pasi na kufunga bao langu bora zaidi la Everton. Nitawaeleza
baadaye wanangu kuhusiana na hilo.
Swali: Vipi kuhusu Steven Pienaar wa Afrika Kusini?
Osman: Mmoja wa wachezaji bora niliowahi kucheza nao. Pienaar alikuwa na kipaji hasa na uwezo wake ulikuwa juu hadi unashangaza.
Swali: Nini unakikumbuka kwake?
Osman:
Uwezo uwanjani lakini mtu mwema nje ya uwanja. Nafurahi leo nipo
Tanzania si mbali sana kutoka Afrika Kusini kwao Steven (Pienaar).
Swali: Hauna umbo kubwa sana, lakini ulikuwa matata na mwenye mafanikio. Vipi uliweza kufanikiwa?
Osman:
Ahsante kwa kung’amua kuwa sina umbo kubwa (kicheko). Ni kweli, muda
wote naocheza nao walikuwa na maumbo makubwa na niliwaangalia namna hii
(anaangalia juu kutoa mfano).
Lakini
kawaida ukishindwa njia hii, unatumia nyingine. Nilijaribu kutumia
wepesi wangu au kuusoma mchezo haraka kuliko wengine. Nilichotaka ni
kufanya vema zaidi ya wapinzani wangu, ndiyo maana nilifika huku kwa
kuwa nilitaka kushinda.
Mahojiano hayo hayakuwa marefu kwa kuwa walitakiwa kuondoka kuwahi ndege kwa kuwa wanarejea England.
Everton
imewahi kubeba makombe tisa ya Ligi Kuu England, matano ya Kombe la FA
pia ubingwa wa Ulaya mara moja lakini imekuwa ikipata shida kubeba
ubingwa tena. Mara ya mwisho ubingwa England ilikuwa msimu wa 1986-87.