MAYANJA AMEINOA TAIFA STARS DAKIKA 420 HUKO MISRI
Mpaka
leo asubuhi Juni 2, mwaka huu, Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya
Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga pamoja na wenzake katika benchi la
ufundi, wamekinoa kikosi hicho kwa dakika 420 ndani ya Uwanja wa
mazoezi wa Kituo cha michezo cha Tolip yaani Tolip Sports City hapa
Alexandria, Misri.
Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mayanga, Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti kutoka Kampuni ya Bia ya SBL itafanya mazoezi yasiyopungua dakika 1,500 katika kambi iliyoanza Mei 31, 2017 usiku na kufikia kikomo Juni 7, mwaka.
Siku ya kwanza ya kambi Mei 31, mwaka huu Kocha Mayanga alianza na dakika 120 za mwanzo baada ya kusafiri salama kutoka Tanzania hadi hapa Misri.
Kila
siku Taifa Stars ina programu mbili ambako asubuhi timu inafundishwa
kwa dakika 90 uwanjani kwa mazoezi mbalimbali na kwa programu ya usiku
ni dakika 120 ambako huanza saa 3.00 (saa 2100) usiku na kumaliza saa
5.00 (saa 2300) usiku kwa saa za hapa Misri.
Kwa
msingi huo, Kocha Mayanga kwa kusaidiana na benchi lake la ufiundi,
anakionoa kikosi hicho kwa takribani saa 25 kwa wiki, kabla ya kurejea
nyumbani. Timu itarudi Tanzania usiku wa kuamkia Juni 8, mwaka huu.
Ikiwa nyumbani Tanzania, Mayanga atawanoa tena kwa dakika nyingine 180 tayari kabisa kuivaa Lesotho Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mchezo huo umepangwa kuanza saa 2.00 usiku.
Mchezo
dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa
Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za
Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika
Cameroon.
Mbali
ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na
Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa
katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza
mwenendo wa mazoezi kwa saa 300 za mwanzo, Kocha Mayanga amesema:
“Nafarajika vijana wangu wameendelea kufunguka. Hapa hawana usumbufu wo
wote, ni mazoezi na kupumzika kulingana na ratiba na chakula.”
Mazoezi
ya Mayanga hayathiri maendeleo ya mwili wa binadamu kadhalika nguzo ya
funga kwa wale ambao wako kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,
kwani ratiba huonyesha huanza kunolewa kuanzia saa 12.00 alfajiri - saa
mbili baadaye baada ya daku (Uhudumiwa daku kabla ya saa 11.00
alfajiri), lakini pia saa 3.00 usiku ikiwa ni saa mbili baada ya
kufuturu (Futari ni saa 12.45 jioni).
Ikiwa
hapa kambini, timu hupata huduma zote kwa upande wa chakula na
wachezaji wana faraja ya kizalendo kuitumikia timu yao ambayo ina
mtihani dhidi ya Lesotho wakijenga imani kabisa kwamba watafanikiwa.