MAXIME; SHUJAA MWINGINE ASIYEKUBALI KUFELISHWA NA WANAOPENDA KUFELISHA
Na Saleh Ally
KAMA
wewe ni mpenda soka, lazima utakuwa umewahi kusikia zile tuhuma ambazo
amekuwa akisukumiwa Kocha Mecky Maxime wa Kagera Sugar kuwa ni mtu mbaya
na amekuwa akipewa hongo ndiyo maana timu anazofundisha hazifanyi
vizuri.
Ushahidi
wa hilo ni yale mabango ambayo mashabiki wa Kagera Sugar waliingia nayo
uwanjani, wakieleza wazi hisia zao kwamba Maxime anapaswa kuondoka.
Kama ilivyo kwa baadhi ya waandishi wasiolijua jina lake sahihi,
mashabiki hao walitumia Mexime.
Mabango
hayo yalikwenda moja kwa moja kuwa Maxime anauza mechi na pamoja na
kufanya hivyo amekuwa akiwasingizia wachezaji. Hakuna hata mmoja kati ya
hao mashabiki aliyekuwa na uthibitisho kuhusiana na hilo lakini
lilikuwa ni shambulizi la moja kwa moja kwa kocha huyo kijana Mtanzania.
Mashabiki
mara nyingi hawana huruma, huangalia matakwa yao na kitu cha kwanza
kwao huwa ni furaha ya mioyo yao. Inapokosekana, kila mmoja huwa ni
adui.
Maxime
alionekana hafai kwa kuwa Kagera Sugar ilipoteza mechi yake dhidi ya
Yanga baada ya kufungwa mabao 6-2 ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba.
Ilikuwa
ni mechi ya 11 ya Kagera Sugar katika msimu na katika mechi 10
zilizopita, Kagera Sugar ilikuwa imeshinda sita, sare tatu na kupoteza
mbili dhidi ya Simba na Toto African.
Kufungwa
na Yanga, likawa ni kosa kubwa ambalo liliwasahaulisha mashabiki hao
ushindi mara sita katika mechi 10. Baada ya mechi dhidi ya Yanga, Kagera
Sugar ikapoteza mechi iliyofuata dhidi ya Azam FC kabla ya kushinda
dhidi ya Mbao FC na Ruvu Shooting.
Ukiangalia
msimamo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara, Kagera Sugar imeshika nafasi ya
tatu nyuma ya Simba na Yanga zilizofungana kwa pointi 68 kila moja.
Azam
FC ambayo imekuwa mzoefu wa ‘Top 3’, safari hii imedondoka hadi nafasi
ya nne na Kagera Sugar wanafuta ubabe wa timu za Dar es Salaam na Top 3
kama ambavyo Mbeya City imewahi kufanya na kuonekana ni shujaa na kiboko
cha vigogo.
Rekodi
ya misimu mitano iliyopita inaonyesha Kagera Sugar haijawahi kushika
nafasi aliyonayo Maxime msimu uliopita. Maana iko hivi; msimu wa
2011-12, Kagera Sugar ilimaliza katika nafasi ya saba, 2012-13 (nafasi
ya nafasi ya 4), 2013-14 (nafasi ya 6), 2014-15 (nafasi ya 6), 2015-16
(nafasi ya 12). Kumbuka huu ni msimu wake wa kwanza Kagera Sugar.
Msimamo
unaonyesha baada ya Simba na Yanga zilizoshinda mechi 21 kila moja,
Kagera Sugar ndiyo inayofuatia kwa kushinda mechi nyingi zaidi ambazo ni
15. Azam FC ni ya nne baada ya kushinda 14.
Huenda
kukawa na hofu, kwamba iwapo Simba itashinda malalamiko iliyopeleka
Fifa, maana yake mambo yatabadilika na Kagera Sugar itateremka hadi
nafasi ya nne. Azam FC itapanda hadi nafasi ya tatu.
Lakini
hii bado haizuii ubora wa Maxime kama kocha uwanjani kwa kuwa kikosi
chake kitakuwa kimeonyesha ubora kiufundi na yeye kama kocha ameshindana
na presha isiyokuwa na sababu, kutoka kwa mashabiki wenye mihemko na
walioshindwa kujiendesha kwa kutafakari mambo kabla ya kujifunza au
kufanya ung’amuzi na kupata uhakika.
Wakati
fulani niliwahi kusimulia, nilikutana na mashabiki wa Simba wasiojua
kufuatilia mambo. Walianza kunizomea na sikujua sababu, lakini sikuwa na
hofu kwa kuwa nawajua mashabiki wengi wa soka ni watu wa kukurupuka.
Lakini
mwisho, nikagundua kuwa walikuwa wakinizomea kwa kuwa siku moja kabla,
Ally Saleh wa Zanzibar alihojiwa na kusema Emmanuel Okwi anapaswa kuwa
mchezaji halali wa Yanga na si Simba. Yeye ni wakala anayetambuliwa na
Fifa, hivyo alieleza alichoamini.
Hata
angekuwa ni Ally Saleh, pia hakupaswa kuzomewa badala yake kama kuna
mtu angekuwa ana hoja, angeanzisha. Kuzomea tu kwa maneno ni kutaka sifa
usiyostahili na mbaya zaidi unakuwa huna kichwa kizuri cha kujenga
hoja.
Waliokuwa
wakinizomea wakidhani mimi ni Ally Saleh, walikuwa ni sawa na wale
waliokuwa wakimsakama Maxime na mambo ambayo hawana uhakika nayo.
Hawajui ukweli uko wapi, ili mradi ni kufuata mkumbo tu na wanakuwa
msitari wa mbele kuzomea ili waonekane wajanja.
Kawaida
katika makundi ya mashabiki wa soka, wanaopiga kelele sana ndiyo
huonekana ni watu wanaojua sana. Kitu kibaya zaidi, wengi wanaotaka
kuonekana wanajua sana huwa hawajui mambo na hupenda kupiga kelele tu.
Sasa
Maxime anathibitisha mambo kwa vitendo, anakwenda kuchukua nafasi ya
tatu akiwa na Kagera Sugar ambayo kushika nafasi kama hiyo hata wengine
walikuwa hawajaanza kuishangilia.
Leo
Kagera Sugar imemaliza katika nafasi ya tatu, wewe ni shabiki na
unakumbuka siku ile ulibeba bango la kumdhihaki kwa maneno makali.
Unajisiakiaje leo? Unaendelea kufurahia mafanikio hayo ya Kagera Sugar?
Wewe
shabiki, ulisema maneno mabaya dhidi ya Maxime ukitaka aondoke,
ukaamini kile ulichoambiwa na mtu aliyeambiwa na yule ambaye hakuwa na
uhakika. Leo unajivunia mafanikio hayo?
Vipi
mashabiki wanakuwa wepesi kulishwa maneno, wanabugia na kuanza
kuyasambaza bila ya kuchunguza. Vipi unakubali kuitwa mtu mzima ambaye
kila unachopewa unameza na kuanza “kumwaga” tena ukionekana una jazba
kweli utafikiri una uhakika!
Maxime
ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, mmoja wa manahodha waliofanya
vema, waliocheza Taifa Stars na Kili Stars zikiwa na njaa. Hata vipi,
bado anastahili heshima yake kama unavyoona mashabiki wa Madrid
wanavyoweza kusimama na kumshangilia Xavi Hernandez au Iniesta kwa
sababu ya utaifa wa Hispania na ubora wa kazi zao.
Ninaamini
kuna watu wengi sana walikata tamaa, huenda leo wangeweza kuwa mbali
lakini walikatishwa tamaa na maneno ya mashabiki ambao wengi
wanayoyasambaza huwa hawana uhakika na wanachokitoa kwa kuwa hujazwa na
wenye malengo yao, nao wakaenda kupayuka tu.
Wengi
hawana nia mbaya, lakini hujikuta wakisambaza maneno kwa kuwa tu
wangependa kuwa wa kwanza kuonekana katika jamii wanajua jambo fulani.
Lakini mara nyingi linakuwa si sahihi.
Wakati
fulani, nilikutana na shabiki mmoja wa Simba, hakika alinifurahisha.
Badala ya kunilaumu, aliweka hoja mezani. Kwamba “Vipi ulisema Rage
alikula fedha ya Okwi na sasa imelipwa?” Mwisho tulimaliza tukiwa
tumeelewana kwa kuwa tulikwenda hoja kwa hoja nikimkumbusha kila jambo,
mwisho akakubali kwa kuwa nilimpa siku za kufuatilia.
Nilimueleza
sikuwahi kuandika Rage kala fedha, badala yake hoja yangu ilikuwa
amekurupuka kwa kuwa alipitisha ITC itolewe Simba ikiwa haijalipwa.
Alionyesha hakuwa makini na ndiyo maana juhudi za Zacharia Hans Poppe
kwenda Fifa zimezikomboa zile fedha. Siku tatu nilizompa akalete
maandiko yangu yoyote kuwa Rage kala zile fedha, ziliishia kwenye kile
nilichomuambia.
Una
hoja, una mawazo? Basi vizuri mueleze mtu kwa njia nzuri na kwa kuwa
alichoweka mezani ni hoja, mnaweza kujadili na kupata jambo sahihi.
Maxime
amegoma kukatishwa tamaa, makocha wengine hasa wazalendo wajifunze
kwake kwamba mashabiki wakati mwingine wanakuwa sumu na kuwasikiliza
sana ni kujiondoa katika njia sahihi.
Vizuri
kujipima, kama utaona unakosea, basi ukajirekebisha. Kama haukosei basi
endelea na kilicho sahihi ili kumaliza na kilicho sahihi. Bravo Maxime.
MSIMAMO
Ligi Kuu Tanzania Bara
P W D L F A PTS
1. Yanga 30 21 5 4 57 14 68
2. Simba 30 21 5 4 50 17 68
3. Kagera 30 15 8 7 33 29 53
4. Azam 30 14 10 6 36 20 52
5. Mtibwa 30 10 14 6 33 32 44
6. Stand 30 9 11 10 25 26 38
MECHI ZA KAGERA LIGI KUU
MZUNGUKO WA KWANZA
Kagera Sugar 0-0 Mbeya City
Kagera Sugar 0-0 Stand United
Kagera sugar 1-0 Mwadui Fc
Ndanda Fc 0-0 Kagera Sugar
Mtibwa Sugar 2-0 Kagera Sugar
African Lyon 0-2 Kagera Sugar
Kagera Sugar 2-0 Prisons
Kagera Sugar 0-2 Toto Africans
Majimaji FC 0-1 Kagera Sugar
Simba 2-0 Kagera Sugar
Jkt ruvu 0-1 Kagera Sugar
Kagera Sugar 2-6 Yanga
Kagera Sugar 2-3 Azam FC
Mbao FC 0-2 Kagera Sugar
Kagera Sugar 3-1 Ruvu Shooting
MZUNGUKO WA PILI
Mbeya 0-0 Kagera
Mwadui 2-1 Kagera
Stand 0-1 Kagera
Kagera 2-0 Ndanda
Kagera 2-1 Lyon
Kagera 2-1 Mtibwa
Prisons 0-0 Kagera
Toto 1-1 Kagera
Kagera 1-0 Majimaji
Kagera 2-1 Simba
Ruvu 1-1 Kagera
Kagera 0-0 JKT Ruvu
Yanga 2-1 Kagera
Kagera 2-1 Mbao
Azam 0-1 Kagera