SERIKALI KUANZISHA MFUKO WA MAENDELEO YA SANAA


Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika kikao cha nane cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 leo Mjini Dodoma Aprili 18, 2017.

Na Daudi Manongi ,Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo inaendelea na mchakato wa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa ili kusaidia kuinua kipato,kuongeza tija na kukuza uwezo na weledi kwa Wasanii nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi, Anastazia Wambura wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge Mjini Dodoma.

“Serikali inategemea kuweka utaratibu mzuri wa upatikanaji fedha na hivyo kuwawezesha Wasanii kuzalisha kazi bora za Sanaa zenye kukidhi viwango vya masoko ya ndani na nje ya nchi”, Alisema Mhe.Wambura.

Aidha amesema katika kipindi hiki ambacho Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa unaandaliwa Serikali inashauri Halmshauri zote ziwasaidie vijana wanaojishughulisha na Sanaa kwa kuwapa mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa ajili ya mitaji kutoka kwenye asilimia 10 ya mapato ya kila Halmashauri kwa kuwa Sanaa pia ni sehemu ya ujasiriamali na ni chanzo kikubwa cha ajira kwa Vijana nchini kwa sasa.

Akizungumzia suala la haki miliki amesema kupitia Bodi ya Filamu,COSOTA na BASATA zimeendelea kuwaelimisha wasanii wa fani mbalimbali kusajili kazi zao ili ziweze kutambuliwa ,kupata udhibiti na ulinzi kutokana na wizi wa kazi za sanaa.Aidha Serikali inaendelea kushughulikia migogoro na biashara haramu ya kudurufu kazi za sanaa ili wasanii waweze kuongeza kipato chao.

“Haki na maslahi ya wasanii yanalindwa kwa Sheria Na.7 ya mwaka 1999 ya Hakimiliki na Hakishiriki,Sheria Na.4 ya Filamu na Michezo ya kuigiza ya 1976 na Sheria Na.23 ya Baraza la Sanaa la Taifa ya 1984 na Serikali inaendelea na mabadiliko ya Sheria hizi ziendani na wakati Alisema”, Mhe.Wambura.

Serikali inaendelea na Urasimishaji wa Tasnia ya Filamu na Muziki ambapo kazi za wasanii hawa zinawekewa stempu za TRA ambazo huwezesha kubaini nakala halisi.
Powered by Blogger.