NAIBU SPIKA APIGA MARUFUKU MASUALA YA USALAMA WA TAIFA KUJADILIWA BUNGENI
Sanga
aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni 68 (7) pamoja na 64 A,B,C,
alisema ndani ya Bunge yameongelewa mambo yanayohusu mahakama, usalama,
mauaji na kutekwa.
“Nilikuwa nadhani kupitia kanuni hizi naomba mwongozo wako nini kazi ya Bunge mheshimiwa naibu spika,” alisema.
Mwongozo
huo uliibuka baada ya Mbunge wa Viti Maalum CCM, Angelina Malembeka
kuwataka wabunge waliosema kuna orodha ya wabunge 11 wanaotakiwa kutekwa
kuwataja majina yao.
Hoja
ya Malembeka ilimlenga Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe
ambaye siku za karibuni aliliambia Bunge kwamba ameambiwa na mmoja wa
mawaziri kuwa kuna wabunge 11 watatekwa na Usalama wa Taifa.
Malembeka
alitoa hoja hiyo wakati akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi
ya Rais, Tamisemi na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Hata
hivyo, mwongozo wa spika ulioombwa na Sanga ulizima kiu ya Malembeka
aliyetaka kumbana Bashe ataje majina ya wabunge hao 11, badala ya kutaja
idadi pekee.
Akijibu
mwongozo wa Sanga, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliamua kupiga
marufuku masuala ya Usalama wa Taifa kujadiliwa bungeni.
Dk Tulia alisema wanaotaka kufanya hivyo wawasilishe hoja mahsusi kwa kufuata Kanuni za Kudumu za Bunge.
Awali, Malembeka alisema ni vizuri Usalama wa Taifa wakaongezwa fedha, mbinu mpya na vifaa ili kurahisisha utendaji wao wa kazi.
“Kutwa
mtu anatuma ujumbe kwenye simu kwa rafiki yake eti nimetekwa nyara,
waulizeni waliotekwa hiyo simu wamepata wapi ya kutumia huo ujumbe kuwa
wametekwa?
“Kutekwa nyara si mchezo, waulizeni wenzenu waliotekwa
watawaambia
si mchezo. Na hao wanaojifanya usalama feki naomba mheshimiwa waziri
uwashughulikie kwa sababu sasa mtu akishakata ‘panki’ lake akavaa kaunda
suti yake anatoa kitambulisho anasema mimi Usalama wa Taifa.
“Usalama wa Taifa mchezo! Mtu anajizungusha zungusha
anawatisha
watu mtaani unasema Usalama wa Taifa sasa wale wanaojifanya Usalama wa
Taifa na kuogopesha watu mtaani washughulikiwe,” alisema.