MSANII WA NYIMBO ZA INJILI JELA MIEZI SITA KWA KUMUITA MTOTO WA MIAKA 9 KUWA NI MCHAWI
Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, imemuhukumu kifungo cha nje cha miezi sita
na kulipa faini ya Sh1 milioni, Aman Mwasote baada ya kutiwa hatiani kwa
kumwita mtoto wa miaka tisa kuwa mchawi.
Mwasote, ambaye ni mwimbaji wa nyimbo za Injili alishtakiwa kwa kutoa
kauli kuwa mtoto huyo huwaloga wanafunzi na walimu alipokuwa kwenye
mkutano wa injili.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi, Venance Mlingi aliyesema
mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa
upande wa Jamhuri kwamba, Mwasote alitenda kosa hilo.
Awali, Wakili wa Serikali, Xaveria Makombe alidai mshtakiwa alitenda
kosa hilo Septemba 20, mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Kalobe, akiwa
kwenye mkutano wa hadhara wa Injili.
Hakimu Mlingi alisema mshtakiwa atatumikia kifungo cha nje kwa kufanya
shughuli za kijamii na Aprili 20 atatakiwa kufika mahakamani ili
apangiwe shughuli ya kufanya.