Jovina Bujulu
Kuwepo
na mfumo wa stakabadhi ghalani kumekuwa ni mkombozi pekee kwa wakulima wadogo na wa kati kwa kuwawezesha kupata bei nzuri ya mazao
yao, ukilinganisha na bei zilizokuwa zinatolewa na wafanyabiashara wanaponunua
mazao yakiwa shambani kwa kutumia vipimo ambavyo sio sahihi.
Taarifa
iliyotolewa na bodi ya usimamizi wa
Stakabadhi za Ghala imesema kuwa
kabla ya mfumo huo kuanza
wakulima walikuwa wakipunjwa bei ya mazao na wafanyabiashara na kutolea mfano zao la
korosho ambapo katika msimu wa 2015/2016, kilo moja ya korosho ilinunuliwa kwa
shilingi 2900 na msimu wa 2016/2017 bei ilipanda na kufikia shilingi 4,000 kwa
kilo ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 15.9.
Mfumo
huo umewanufaisha wakulima kwa kutumia ghala ambazo ziliachwa kwa muda mrefu
bila matumizi ambazo zimekuwa na tija kwa wakulima.
Kupitia
ghala hizo zenye ujazo wa kuanzia tani 200 hadi 5000 na kuendelea wameweza
kuhifadhi mazao yao vizuri na kwa ubora
unaotakiwa kwa matumizi ya sasa nay a baadaye.
Aidha,
mfumo huo umeongeza ajira kwa wakina mama na vijana hasa katika maeneo ya
kuchambua, kupokea na kupanga mazao ghalani. Vijana wengi wameajiriwa kwa kazi
ya kushusha, kupanga na kupakia mazao na wameweza kujiajiri katika kilimo baada
ya kuona mfumo huo unavyofanya kazi vizuri
na kuwa na uhakika wa soko la mazao yao.
Wakulima
pia wamepata mafanikio kwa kuwa na uhakika wa vipimo vya mazao yao
yanayohifadhiwa ghalani kupimwa kwa
kilogramu na si vinginevyo ambapo kabla
ya mfumo huo wakulima walikuwa wakiibiwa mazao yao kutokana na matumizi ya vipimo ambavyo si sahihi.
Kwa
kuhifadhi mazao yao katika ghala zenye leseni, wakulima wamekuwa wanatumia
mazao hayo kama dhamana ya kupata mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za
fedha. Hii imewezekana kutokana na wakulima hao kujiunga katika umoja kupitia
vikundi au vyama vya ushirika.
Wafanyabiashara
pia wameneemeka na mfumo huu, ambapo kwa sasa wameweza kupunguza gharama za
kufuata mazao maeneo mbalimbali mazao yanapatikana kwa wingi badala yake mazao
hayo wanayapata katika eneo moja kkwenye ghala zilizosajiliwa na hivyo kuondoa
hatari ya kuibiwa pesa zao na madalali wasio waaminifu.
Mfumo
huo pia umekuwa na faida kwa bodi za
mazao katika kuandaa bajeti za mahitaji ya pembejeo na kuongeza ili kuboresha na kuongeza uzalishaji.
Aidha,
mfumo huo umechochea na kuharakisha uanzishwaji wa soko la bidhaa nchini,
kutokana na kuwepo kwa bidhaa zenye ubora na zinazopatikana kwa wakati. Bodi ya
Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, inatoa
wito kwa wakulima kuunga mkono uhamasishaji
wa matumizi ya soko hilo ili kuongeza tija na kasi ya kukuza biashara ya mazao ya kilimo hapa
nchini.
Mfuko
wa Stakabadhi Ghalani ulianza mwaka 2000 ukifadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa
Bidhaa. Lengo la mfuko huo ni kuwezesha wakulima kufaidika na ongezeko la bei katika
msimu wa mazao, kuongeza mapato ya wakulima na kuboresha kipato chao ikiwa ni
pamoja na kuwapa wakulima nguvu ya soko kwa kuhamasisha utumiaji
wa vikundi vya wakulima na ushirika.
|