Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi baada ya kuzungumza nao kwenye makazi yake,
Oysterbay jijini Dar es salaam Januari
24, 2017.
Picha/Habari na Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU amewataka Wajumbe
wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) wakutane na wamiliki
wa taasisi za kifedha ili kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo yenye gharama
nafuu.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Januari 24, 2017) wakati alipokutana na wajumbe wa
baraza hilo katika Makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu amesema ni vema wajumbe hao wakakutana na wamiliki wa taasisi hizo za
kifedha ili kuwasaidia wananchi kupata mikopo yenye masharti nafuu
itakayowawezesha kukuza uchumi wao.
“Baraza
likutane na wamiliki hao na kuzungumza namna sahihi ya kuwezesha kutoa mikopo
ya masharti nafuu. Pia tuangalie taasisi hizo zinatuasadiaje sisi kama
Serikali kuwawezesha Watanzania kupata mikopo ya masharti nafuu,” amesema.
Amesema
wananchi wanahitaji kuona ni namna gani Serikali imejipanga kuwawezesha wao
kiuchumi, hivyo baraza litoe muelekeo wa namna ya wananchi watakavyoweza kufuga
na kulima kitaalam ili waweze kupata tija.
Waziri
Mkuu amesema asilimia 80 ya wananchi wanajishughulisha na kilimo kama njia
sahihi ya kuboresha uchumi. Pia ufugaji unaweza kusaidia jamii ya wafugaji
kupata tija, hivyo baraza liwasaidie kwa kuwapa mbinu sahihi za kuboresha
ufugaji wao.
Awali
Mwenyekiti wa baraza hilo, Dk. John Jingu alisema baraza
lilizinduliwa Januari 8, 2017 na walikubaliana kuanza kazi katika maeneo
ya kipaumbele yatakayokuwa na tija kwa wananchi ambayo ni kilimo, sanaa,
ufugaji na uvuvi.
Alisema
wanaamini kuwa uwezeshaji katika maeneo hayo utaleta matokeo ya haraka kwa
wananchi wengi kwa kuwa shughuli zao nyingi zimejikita katika maeneo hayo.
Dkt.
Jingu alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kutafuta mbinu zitakazoweza kutatua
changamoto kubwa zinazowakabili ambazo ni pamoja na ukosefu wa mitaji na
masoko ya uhakika kwa mazao yao.
Alisema
moja ya mbinu wanazotarajia kutumia ili kuleta mabadiliko ya haraka na yenye
tija ni kuimarisha uhusiano katika sekta bukwa na za kati na vikundi vya
wazalishaji wadogo.