WATUMISHI WA UMMA WAONDOLEWA HOFU KUHAMIA DODOMA.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Mathew John Mtigumwe
akisisitiza jambo wakati wa kikao cha pamoja na wafanyakazi wa wizara
hiyo.
Na Mathias Canal
Watumishi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi wakimsikiliza kwa makini Katibu mkuu wa wizara hiyo Mhe Mhandisi Methew Mtigumwe
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Mathew John Mtigumwe
amewaondoa hofu watumishi wa wizara yake kuhusu zoezi la serikali
kuhamia
Dodoma kuwa litafuata misingi na stahili za watumishi kwa mujibu wa
kanuni za
utumishi wa Umma.
Mhandisi Mtigumwe alitoa kauli hiyo jana wakati wa kikao maalumu cha kuhusiana na
uamuzi wa serikali kuhamia Makao Makuu ya Nchi mkoani Dodoma kilichokuwa na
lengo la kujadili kwa pamoja namna ya utendaji kazi katika wizara hiyo sambamba
na kutoa utaratibu utakavyokuwa kuelekea mjini Dodoma.
Mtigumwe alibainisha kuwa Awamu ya Kwanza ya uhamisho
utawahusisha watumishi 88 kutoka Idara Kuu ya Mazao, ambapo katika mchakato huo
watumishi 41 watahamia Dodoma kuanzia tarehe 14 – 15/2/2017 na wengine 47
waliobaki watahamia muda wowote katika kipindi cha kuanzia mwezi Februari hadi kufikia
mwezi Juni.
Mtigumwe aliwaeleza watumishi hao kuwa maandalizi ya ofisi za Wizara ya kilimo zilizopo mjini Dodoma zinaendelea vizuri na tayari baadhi ya maeneo yamekamilika huku mengine yakiendelea kukamilishwa ili kukidhi matakwa kwa ajili ya watumishi wote watakapohamia mjini Dodoma.
Uamuzi wa Watumishi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kuhamia mjini Dodoma ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kuitaka Serikali yote kuhamia Dodoma ili kutekeleza uamuzi uliofikiwa tangia miaka ya 70 na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutambua na kutangaza kuwa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi.