SUMAYE AMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KUSIMAMIA SERA ZA CHADEMA
Wakati Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli akitekeleza masuala
mbalimbali aliyowaahidi Watanzania, ikiwa ni pamoja na kurejesha
uwajibikaji na kupambana na ufisadi, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick
Sumaye amesema hashtushwi na utendaji huo wa rais, kwani amekuwa
akitumia baadhi ya hoja na mikakati ya Chadema kuongoza nchi.
Akizungumza wakati wa kumnadi mgombea wa udiwani katika kata ya Isagehe
wilayani Kahama, Sumaye ambaye alijiunga Chadema Agosti mwaka juzi baada
ya kuachana na CCM, alisema mengi anayofanya rais ni sera za Chadema
ila chama hicho cha upinzani hakikuwa na sera ya kubana fedha.
Hata hivyo, Sumaye ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema hakuweka
wazi hoja na mikakati ya Chadema inayotekelezwa na Rais Magufuli ambaye
tangu aingie madarakani ameweka msimamo katika suala la kubana matumizi
ya Serikali, kudhibiti watumishi hewa na safari za ndani na nje zisizo
na tija na rushwa.
Katika mkutano huo ambao pia Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa
alihutubia, Sumaye alisema kama wananchi, wangemchagua Lowassa kuwa
Rais, angewaletea neema ya hali ya juu kwa kuwa angekuwa na misingi
katika sera anazozitekeleza.
“Mmechagua Rais mzuri (Magufuli), lakini anafuata sera za chama chetu
(Chadema) ambazo tungezitumia kama tungekuwa madarakani. Wananchi wa
Kanda ya Ziwa mnatakiwa kumtumia Rais Magufuli ili kufanikisha malengo
yetu,” alisema huku akisisitiza kuwa hata Lowassa wananchi wangeweza
kumtumia kufanikisha malengo yao.
Huku akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, John Luzinga, Sumaye
aliwataka wananchi kutofanya makosa tena ya kuichagua CCM, ili wasije
kujuta kwa maelezo kuwa watalazimika kuchagua diwani mwingine mwaka
2020.
Alisema Chadema kinaendeshwa kwa kufuata misingi ya demokrasia, huku
akikosoa vyama kubanwa wakati nchi iriuridhia mfumo wa vyama vingi vya
siasa.
Akizungumzia sababu za kuhama CCM, alisema kulitokana na nchi kukumbwa
na hali mbaya ya uchumi sambamba na kukosekana kwa utawala bora.
“Serikali pamoja na kubana matumizi, hali ya uchumi imekuwa mbaya.
Inatakiwa kuachia fedha ili kuwafikia wananchi waweze kumudu ugumu wa
maisha unaowakabili kwa sasa. Haiwezekani kila Serikali isijifunze
katika hili wakati hata wataalamu wanazungumza na kushauri masuala
mbalimbali,” alisema Sumaye.
Alisema kitendo cha halmashauri tatu za wilaya ya Kahama kuongozwa na
CCM, huku diwani mmoja tu ndio akiwa wa Chadema, kitawafanya wananchi
hao kukosa watu sahihi wa kuwasemea mambo yao.
Uchaguzi katika kata hiyo utafanyika Januari 22 sambamba na kata nyingine 21 katika maeneo mbalimbali nchini.