MBUNGE LIJUALIKALI ALIYETUPWA JELA MIEZI SITA KUENDELEA NA UBUNGE
Mjadala umeshika kasi mitaani, mitandaoni na kila mahali baada ya
Mahakama ya wilaya ya Kilombero kumhukumu kutumikia kifungo cha miezi
sita jela bila faini Mbunge Wa jimbo la Kilombero Mhe. Peter Lijualikali
(30) kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki katika maeneo ya
ukumbi Wa halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Mbunge huyo, akiwa mshtakiwa namba moja pamoja na mwenzie Stephano Mgata
(35) walitenda kosa hilo Machi 1, 2016 saa 4 asubuhi Kwenye kikao cha
Baraza la Madiwani katika eneo la Kibaoni ukumbi wa halmashauri ya
wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Imeelezwa kuwa kwa pamoja walifanya fujo kinyume na kifungu namba 89
kifungu kidogo cha kwanza B, cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama
ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ambapo washtakiwa walikana mashtaka na
hivyo kufanya kesi kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na upande wa
mashtaka ukathibitisha bila kuacha shaka.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhan
ameibuka na kukata kiu ya wananchi ya kutaka kujua endapo baada ya
hukumu hiyo Mhe. Lijualikali ataendelea kuwa mbunge.
Akihojiwa na TBC One wakati wa taarifa ya habari ya saa mbili jana
usiku, Bw. Kailima aliweka bayana kwamba mbunge huyo ataendelea na
wadhifa wake kwa kuwa sheria inasema ili kupoteza kiti ni lazima uwe
umepewa adhabu ya kifungo cha ZAIDI ya miezi sita jela.
"Ibara ya 67(2)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza
mambo yanayotoa sifa ya kuwa Mbunge kutoka madarakani ni kifungo cha
zaidi ya miezi sita jela. Huyu bwana kafungwa miezi sita kwa hiyo bado
hajapoteza sifa za kuendelea kuwa mbunge akiwa gerezani na baada ya
kumaliza kifungo chake", alisema Bw. Kailima.