MADIWANI WA CHADEMA WASUSIA POSHO
MADIWANI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, wamesusa posho za vikao vya kamati vinavyoendelea kwa madai kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Magreth John amezipunguza bila ridhaa yao.
Madiwani hao kutoka kamati za Elimu, Afya, Maji na Uchumi, Ujenzi na Mazingira wamegoma kupokea posho ya Sh 40,000 kwa kila kikao wakitaka kulipwa posho ya awali ya Sh 82,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, John amekiri kususiwa posho hizo na kuongeza kuwa hatua hiyo inafuatia kufuatwa kwa waraka wa serikali wa mwaka 2007 na 2012 unaoelekeza viwango stahili vya posho kwa madiwani.
Mkurugenzi amesema waraka huo wenye Kumb Na CHB/443/01 wa Novemba 26, 2007 umetaja viwango vya malipo ya madiwani kwa mwezi, posho ya madaraka kwa wenyeviti wa kamati, wenyeviti wa halmashauri za wilaya, manispaa na majiji nchini na kwamba yeye ni msimamizi na hafanyi kwa matakwa yake.
Amesema, kutumika kwa waraka huo kutaisaidia halmashauri kuokoa zaidi ya Sh milioni 60 ambazo zitatumika katika miradi ya maendeleo kama afya, elimu na maji.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Evarist Silayo amesisitiza msimamo wake kwamba posho ya kikao ni Sh 82,000 kama ilivyo kwa halmashauri nyingine mkoani Kilimanjaro ambazo zipo juu ikilinganishwa na Rombo.
“Posho hii tumeikuta ilipitishwa na madiwani wa awamu zilizotangulia lakini pamoja na hilo tulipoingia sisi tulijaribu kuondoa vyakula wakati wa vikao vya kamati... hakuna diwani wa Rombo analipwa posho ya usafiri, madaraka isipokuwa wenyeviti wa kamati na mwenyekiti wa halmashauri,” amesema.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Rombo linaundwa na madiwani 38, wakiwamo 28 wa kata, huku kati yao 37 ni kutoka Chadema na mmoja kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).