Nyabitara
Magori(45)ngariba mkazi wa kijiji cha Mesaga wilayani Serengeti akilia
baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kumkeketa mtoto wa
miaka 16 kwa ujira wa sh 5,000 na kumsababishia madhara,akitoka gerezani
anatakiwa kumlipa fidia ya sh 5 mil,kutokana na madhara
aliyomsababishia
Habari na Serengeti Media Centre
.Ngariba
aliyemkeketa mtoto wa miaka 16 kwa kushirikiana na bibi yake wakazi wa kijiji
cha Mesaga wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara wamehukumiwa kifungo cha miaka 10
kila mmoja na kumlipa fidia ya sh 5 milioni kwa kila mmoja.
Waliohukumiwa
na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ni Nyabitara Magori(45)ngariba
na Nyakaho Nyaisa (64) bibi wa mtoto aliyekeketwa kwa nguvu ili kutimiza mila
za jamii ya Wangoreme.
Akitoa
hukumu katika kesi ya jinai 206/2016 baada ya kusikiliza maelezo ya mwendesha
mashitaka na utetezi wa washitakiwa Hakimu Ismael Ngaile alisema kutokana na
kukithiri kwa vitendo hivyo ambavyo vinasababisha madhara kwa watoto wa kike
lazima atoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
“Kila mmoja
atakwenda jela miaka kumi na mnatakiwa kumlipa fidia mtoto ya sh 5 milioni kwa
kila mmoja kutokana na madhara mliyomsababishia kama ilivyoelezwa na
daktari,”alisema hakimu.
Hukumuhiyo
ni ya pili kutolewa kwa ngariba na
wazazi katika mahakama hiyo iliibua kilio kutoka kwa washitakiwa hao na hofu
kwa washitakiwa wengine wenye makosa kama hayo waliokuwa mahakamani
hapo.
Katika
utetezi wa washitakiwa Nyakaho Nyaisa(bibi wa mtoto) aliiomba mahakama
kumpunguzia adhabu kwa kuwa ni mgonjwa wa kifua kikuu na ana familia
inayomtegemea kwa upande wake Nyabitara Magori aliiambia mahakama kupunguziwa adhabu kwa kuwa ni mjane na ana
familia inayomtegemea.
Mapema
mwendesha mashitaka wa Polisi Jakobo Sanga mbele ya hakimu Mfawidhi wa mahakama
hiyo alisema watuhumiwa walitenda kosa
mnamo oktoba 18 ya mwaka huu katika kijiji cha Mesaga wilayani hapa kwa kumkeketa mtoto wa miaka 16 kinyume cha
sheria .
Alisema
vitendo hivyo ni kinyume cha kifungu cha 169(A)cha sheria kanuni ya adhabu sura
16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Sanga ameileza mahakama kuwa kutokana na maelezo ya shitaka na ushahidi
uliotolewa ikiwemo taarifa ya daktari na mtoto aliyekeketwa aliomba Mahakama
kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine.
|