UHAMIAJI WAZIPIGA MARUFUKU SIMBA,YANGA NA AZAM KUTUMIA WACHEZAJI WA KIGENI
Serikali imevipiga marufuku Klabu za ligi kuu Tanzania hususani Simba,
Yanga na Azam kuwatumia wachezaji wa kigeni mpaka watakapokamilisha
taratibu zao za uhamiaji.
Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya klabu ya Ndanda FC kutuma
malalamiko TFF kwamba Simba iliwatumia wachezaji wake wawili wa kigeni
Daniel Agyei na James Kotei kwa madai kwamba hawana vibali vya kufanya
kazi nchini.
Klabu hizo zimepewa maagizo kwamba wachezaji na makocha wote wa kigeni
ambao hawajakamilisha taratibu za uhamiaji hawatoruhusiwa kuzihudumia
klabu zao hadi hapo watakapokamilisha taratibu hizo.
Idara ya uhamiaji kupitia kwa afisa uhamiaji John Msumule leo alitoa
tamko kwa klabu zote za Ligi Kuu Tanzania bara kutoendelea kuwatumia
wachezaji wake wa kigeni hadi watakapotimiza masharti ya uwepo wao
nchini kisheria na uhamiaji wamezitaka klabu za Simba, Yanga na Azam FC
kuhakikisha wachezaji wake na makocha wao wa kigeni wanapata vibali vya
kufanyia kazi nchini pamoja na kuishi.
Hata hivyo kwa upande wa Yanga wao wachezaji wao wana vibali vya kazi na
vya kuishi nchini isipokuwa makocha wao ndio wana vibali vya kazi
pekee.
Kwa upande wa watani zao wa jadi Simba wao hawajatimiza vigezo hivyo kwa
wachezaji wao wa kigeni na makocha wao, hivyo hawaruhusiwi kuendelea
kuwatumia wachezaji wao ambao hawana vibali mpaka watakapo vipata vibali
ingawa uongozi wa klabu ya Simba ulisema kuwa wachezaji hao
wamekamilika kila kitu.