Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Tundu Lissu, akizungumza na wabunge wenzake baada ya kurudi
bungeni akitoka kutumikia adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili ya
Bunge mjini Dodoma jana.
*****
WABUNGE jana waliendelea kuchachamaa
dhidi ya mawaziri na kusema kuwa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli
imekuwa na matumizi makubwa kuliko kile kinachopatikana, huku wakimtaja
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kuwa ana kiburi na
hashauriki.
Wakati wabunge mbalimbali wakiendelea
kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017/18
na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto
Kabwe (ACT-Wazalendo), ameibua bomu jipya kuhusu matumizi ya Serikali
kwa kipindi cha mwaka mmoja na kusema kuwa kuna tofauti ya Sh bilioni 78
za malipo ya mishahara ya watumishi katika kipindi cha mwaka mmoja.
Wakati Zitto akisema hayo, Mbunge wa
Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alisema licha ya mipango ya maendeleo
kupangwa na Bunge, lakini huenda ikakwama kutokana na kile alichokiita
kiburi cha Waziri Dk. Mpango.
ZITTO
Zitto alisema kuwa pamoja na nia nzuri
ya Serikali kubana matumizi, bado kuna ukakasi kwenye taarifa yake
kuhusu matumizi ya fedha za mishahara kwa watumishi.
“Gharama za watumishi zinazotolewa kila
mwezi na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki pamoja na
zile za Benki Kuu (BoT) zinaonyesha kuanzia Agosti 2014 hadi Juni 2015
Serikali ililipa shilingi bilioni 456. Lakini pia ukiangalia taarifa za
hadi Juni 2016 fedha zilizolipwa ni shilingi bilioni 534, tofauti ikiwa
ni shilingi bilioni 18.
“Wakati Waziri Kairuki akisema katika
taarifa zake kuwa wanaokoa shilingi bilioni 19 za watumishi hewa,
ukichukua hesabu zote hizo kwa kipindi hiki utakuta Serikali imetumia
zaidi ya shilingi bilioni 78. Sasa sijui nani mkweli kati ya waziri au
BoT, hivyo kuna mmoja wao anadanganya umma, ni lazima utolewe ufafanuzi
wa kina katika hili. Je, inakuwaje matumizi yawe juu zaidi wakati hakuna
ajira mpya?” alisema Zitto na kuhoji.
Kuhusu sekta ya elimu ya juu nchini,
mbunge huyo alisema ni jambo la kusikitisha kwa kipindi cha mwaka wa
masomo 2017/18 wanafunzi waliokuwa na sifa za kupata mikopo ya Serikali
ni 65,000 lakini waliopata ni 20,000 tu huku wengine wakikosa.
Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama
cha ACT-Wazalendo, aliponda hatua ya Serikali kutoa mkopo wa elimu ya
juu kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi tu na kuziacha fani
nyingine.
Alisema nchi haiwezi kujengwa na
wataalamu wa sayansi pekee, kwamba ni lazima Serikali iwe na utaratibu
wa kufadhili masomo yote ya elimu ya juu ili wataalamu wa fani nyingine
wapatikane pia.
“Huwezi kujenga uchumi wa viwanda kwa
wanasayansi pekee. Je, hivi utakuwa na kiwanda kwa wanasayansi pekee
bila kuwa na watu wa HR (wataalamu wa rasilimali watu), wahasibu na fani
nyingine.
“Ili tuweze kufika huku, tuwe na
utaratibu wa kutoa na ‘scholarship’ kwenye fani mbalimbali, na hili
suala tulilijadili kwenye kamati kutwa nzima na Waziri Ndalichako
(Profesa Joyce) alikuwepo,” alisema.
Zitto alisema anashangazwa na hatua ya
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mpango kushindwa kusimamia andiko lake
lililochapishwa katika jarida la Repoa, kuhusu hali ya umaskini, ikiwamo
kile alichoshauri kuhusu uongozi na timu ya ushindi.
“Ili kulitekeleza hilo, ni lazima tuwe
pamoja. Lakini sasa Serikali na Bunge hawako pamoja katika mikakati ya
uendelezaji nchi. Serikalini mawaziri hawaelewani, ndiyo maana kila
kukicha utasikia matamko na kutengeneza front pages (kurasa za mbele) za
magazeti. Wabunge na Serikali tujichanganye maana sijui wapi
tunakwenda,” alisema.
CHEGENI
Kwa upande wake, Mbunge wa Busega, Dk.
Chegeni, alisema pamoja na utalaamu alionao Waziri Dk. Mpango, lakini
ili afanikiwe lazima aondoe kile alichokiita kiburi.
“Chukua mawazo ya wabunge fanyia kazi,
haiwezekani tupange mipango kwenye kitabu, lakini utekelezaji wake
hatuambiwi iliyopita ikoje na wapi tumekwama.
“Ninajua Rais Magufuli ana nia njema na
Watanzania, haiwezekani mawaziri kuwa na lugha tofauti. Kupitia mpango
huu fanyia kazi hali ya uchumi, mzunguko wa fedha haupo mitaani na pia
hata masilahi yetu wabunge yabebe.
“Rais anafanya juhudi kubwa ili Watanzania wanufaike na rasilimali zao, nanyi (mawaziri) msaaidieni, acheni kusigana,” alisema.
HECHE
Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John
Heche (Chadema), alisema kuwa uchumi wa nchi hauwezi kwenda kwa maneno
kwani anaona baada ya kutumbuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Charles Kitwanga atakayefuata ni Dk. Mpango.
Heche alisema nchi haiwezi kwenda bila
kuwekeza kwenye elimu, lakini kinachofanywa sasa na Serikali ni kuwatesa
wanafunzi wa elimu ya juu.
Alisema anashangazwa na mawaziri wa
Serikali ya awamu ya tano kutoa kauli za kuwataka vijana wakajiajiri,
huku wao ambao wengine ni maprofesa, madaktari na hata wanasiasa wa
kawaida wamekimbilia kuomba ajira za wananchi.
“Ninashangaa sana kila siku mnasema
vijana mjiajiri, watajiajiri vipi? Na kama nyepesi mbona wewe
umekimbilia huku? Tena wengine ni maprofesa na madaktari. Tena na mama
Ndalichako (Joyce) nilikuwa na kuheshimu kweli ulipokuwa pale Baraza la
Taifa la Mitihani (NECTA) ukionyesha wanafunzi waliochora zombie, lakini
leo wewe ndiyo umechora zombi kubwa ambalo halijapata kutokea.
“Kuna mwingine mnamwita ‘Mzee wa Sound’,
ukimsalimia anaweka mikono mifukoni anakuuliza unataka kiwanda? Sijui
hicho kiwanda amekiweka mfukoni,” alisema Heche.
Na Bakari Kimwanga-Mtanzania DODOMA
|