TABATA KIMANGA JIJINI DAR ES SALAAM WAZUNGUMZIA CHANGAMOTO YA DARAJA INAYOWAKABILI.
Mtoto Juma Ramadhan mwanafunzi wa
darasa la pili katika Shule ya Msingi ya Tabata Kimanga, akiwa amembeba
mdogo wake Sara Sadiki wakati wakipita katika daraja la miti
linalounganisha wakazi wa Tabata Kimanga na Tabata Chang'ombe Dar es
Salaam , ambapo wakazi wa eneo hilo wanaiomba Manispaa ya Ilala
iwajengee daraja la kudumu.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Amani,
Jonathan Mlay akimuonesha mwandishi wa mtandao huu, daraja la miti
wanalolitumia lililojengwa kwa nguvu za wananchi kwa ajili ya
kukabiliana na changamoto hiyo.
Na Dotto Mwaibale.
WANANCHI
wanaoishi mpakani mwa Tabata Kimanga na Chang'ombe katika Manispaa ya
Ilala jijini Dar es Salaam wameomba kujengewa daraja ili waweze kutumia
muda mfupi wa kufika katika maeneo hayo badala ya kupitia Tataba
Mawenzi.
Ombi hilo
wamelitowa Dar es Salaam jana wakati wakizungumza kuhusu changamoto
mbalimbali zilizopo katika eneo hilo ikiwemo ya kujengewa daraja hilo
lililopo Mtaa wa Amani.
Akizungumzia
changamoto ya daraja hilo, mkazi wa eneo hilo Tusekelege Ambonisye
alisema wamekuwa wakitumia muda mwingi wa kuzunguka na gari kupitia
Tabata Bima na kwenda Tabata Chang'ombe lakini kama daraja hilo
linalounganisha maeneo hayo lingejengwa lingewarahisishia" alisema
Ambonisye.
Aliongeza kuwa
adha kubwa waliyonayo ni pale ikinyesha mvua kwani maji yanajaa na
barabara hiyo kushindwa kupitika ikiwa ni pamoja na kuhatarisha maisha
ya watu wanaojaribu kupita kaika eneo hilo.
Alisema
kutokana na adha waliyokuwa wakiipata wananchi wa eneo hilo walikusanya
nguvu na kujenga daraja la miti la muda ambalo linatumika lakini sio
salama kwa watumiaji.
Mjumbe wa
Serikali ya Mtaa huo wa Amani, Jonathan Mlay alisema changamoto ya
daraja hilo ni ya muda mrefu kwani waliwahi kuiwasilisha kwa wabunge wa
jimbo hilo waliopita na wa sasa Bonah Kaluwa lakini bado halijapatiwa
ufumbuzi wowote.
"Kupitia vikao
vyetu vya kamati ya maendeleo ya mtaa changamoto hii tuliipeleka kwa
wabunge waliopita pamoja na huyu wa sasa tupo tunasubiri matokea yake"
alisema Mlay.