|
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kinakusudia kufungua maombi
katika Mahakama Kuu ya kuiomba mahakama hiyo kuiamuru Polisi kuwafikisha
mahakamani watu wanaoshikiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Dar es
Salaam.
Hatua
hiyo inatokana na chama hicho kudai kuwa kuna watu 10 ambao wanashikiliwa
katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central) na Kituo cha Oysterbay vya Dar es
Salaam kwa zaidi ya wiki mbili bila kupewa dhamana ya polisi au kufikishwa
mahakamani.
Kauli
hiyo ya Chadema imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu
wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu yake yaliyo mtaa wa
Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam leo mchana.
Akifafanua
kuhusu Habeas Corpus alisema, ni mamlaka iliyonayo Mahakama Kuu ya kuamuru
mamlaka yoyote ya kiserikali inayomshikilia mtu kumpeleka mtu huyo mahakamani.
Lissu
alisema, vijana hao walikamatwa katika mikoa mbalimbali kwa makosa aliyodai
kuwa ni kujihusisha na haraka za kinachoitwa Umoja wa Kupambana na Udikteta
(UKUTA) pamoja na masuala mengine ya kisiasa.
“Kama
ikifika Jumanne hawajapelekwa mahakamani au hawajapewa dhamana ya polisi,
tutakwenda Mahakama Kuu kufungua maombi ya habeas corpus, imuite IGP au DCI au
Ma-RPC au wakuu wa vituo wanakoshikiliwa hao waeleze kwa kwanini wanawashikilia
hao watu kwa zaidi ya wiki mbili,” alisema Lissu
Lissu
alisema tayari wameshaanza maandalizi ya hati hizo ambazo zitapelekwa Mahakama
Kuu ili iweze kuwaita kati ya Mkuu wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Makosa ya
Jinai (DCI), Makamanda wa Polisi wa Mikoa au Wakuu wa Vituo vya Polisi
wanakoshikiliwa watu hao.
Alifafanua
kuwa alionana na watu hao ambao wamedai mbali na kushikiliwa lakini pia
wamepigwa na kuteswa huku wakidai kuwa wamekuwa wakichukuliwa usiku na
kupelekwa katika eneo lililopo Mikocheni ambako wanateshwa na kurudishwa
polisi.
Alisema
jeshi la polisi linakiuka sheria na haki za binadamu kwa kuwashikilia watu hao
kwa muda mrefu bila kuwapa dhamana au kuwafikisha mahakamani kwa ajili ya
kusomewa mashitaka.
|