Mama Maria Nyerere Atoa Ushauri Kwa Vijana
Mama Maria Nyerere, amewaasa vijana kuzingatia utamaduni na michezo ili kuweka sawa akili zao.
Amesema michezo hukutanisha watu wengi na kuwawezesha kubadilishana mawazo yenye kujenga katika maisha.
Mama
Maria amesema hayo jana Alhamisi alipozungumza na Mkurugenzi wa Idara
ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbasi nyumbani kwake jijini Dar es
Salaam.
Taarifa
ya Maelezo imesema Mama Maria amesema michezo ni hatua muhimu ya
ukombozi wa fikra kwa vijana kwa kuwa wakiizingatia wataweza kufanya
kazi na kujipatia mahitaji muhimu kama vile chakula na kuondokana na
dhana ya utegemezi.
“Vijana
wamejikita katika mambo maovu, sasa kitakachoweza kusaidia ni michezo
kwa kuwa inawachangamsha, kuwakutanisha na kubadilishana mawazo mazuri
na kwa sasa wanaendelea vyema na masuala haya ya michezo ambayo
yanadumisha pia utamaduni,” amesema.
Mama
Maria, ambaye ni mjane wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere amesema kwa
sasa vijana wameanza kujirudi katika kudumisha utamaduni kwa kuwa
walitaka kupotoka na kuacha utamaduni wao.
Amesema
watoto wanazaliwa bila ukomavu wa akili katika utamaduni, lakini pia
hawapati elimu ya kutosha kutoka kwa wazazi kuhusu utamaduni, hivyo
matokeo yake ni kuishia kuwa na watu wenye tabia za ajabu.
Mama
Maria amesema jukumu la ukombozi wa vijana kutoka katika vitendo vibovu
ni la Watanzania wote kuwaelimisha vijana kuhusu michezo ili kuweka
akili zao sawa.
Amesema
kujitegemea kwa vijana na hasa katika kufanya kazi kutawawezesha
kutimiza ndoto zao na za Taifa lenye kipato cha kati kwa kutegemea
uchumi wa viwanda.